January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Batilda ataka kiwanda cha asali sikonge kuanza kazi

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Sikonge

MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian amemwagiza Mkuu wa wilaya ya Sikonge na Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo kufanya kila linalowezekana ili kiwanda cha kuchakata asali kilichojengwa wilayani humo kinaanza kufanya kazi.

Ametoa agizo hilo jana katika kikao maalumu cha mapitio ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Alisema kiwanda hicho ambacho ujenzi wake umegharimu zaidi ya sh mil 700 ni fursa muhimu sana kwa wakazi wa wilaya hiyo na Mkoa mzima kwa kuwa kitasaidia kuongeza thamani ya zao hilo na kuchochea uchumi wa wananchi.

Alibainisha kuwa licha ya kufungwa mitambo ya kuchakata zao hilo na mazao mengine yatokanayo na nyuki na kufanyiwa majaribio hadi sasa hakifanyi kazi jambo linalowakosesha wananchi fursa nyingi za kiuchumi.

‘Kiwanda hiki kimegharimu fedha nyingi, haiwezekani kikae hivi hivi, nataka kianze kufanya kazi, Mkurugenzi na Mkuu wa wilaya fanyeni kila linalowezekana ili kianze kazi’, aliagiza RC.

Balozi Batilda alisisitiza kuwa wilaya hiyo inaongoza kwa uzalishaji wa asali, hivyo uwepo wa kiwanda hicho ni fursa muhimu sana kwa wafuga nyuki kuzalisha asali ya kutosha, kuichakata na kuuzwa maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Aidha alimwagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo Dkt John Mboya kufuatilia suala hilo kwa ukaribu zaidi na kuhakikisha kinaanza kufanya kazi ili kuwarahisishia kazi wafuga nyuki wa wilaya hiyo na Mikoa jirani ya kuchakata mazao yao.   

Alifafanua kuwa mazao ya nyuki yana soko kubwa sana ndani na nje ya nchi na wageni wengi wameshatembelea kiwanda hicho na kuonesha nia ya dhati ya kununua asali inayozalishwa katika wilaya hiyo na Mkoa mzima wa Tabora.

RC aliongeza kuwa kiwanda hicho kitasaidia kupanua wigo wa utalii wa nyuki katika Mkoa huo na kuongeza thamani ya mazao ya nyuki, huku akibainisha kuwa timu ya watalii kutoka nchini Afrika Kusini itarajia kuwasili Mkoani humo mapema mwakani kwa ajili ya kujifunza shughuli za ufugaji nyuki.  

Katika kikao hicho RC aliagiza kuundwa kwa kamati maalumu ya kupitia hoja zote zilizobainishwa katika taarifa ya CAG na kuzipatia ufumbuzi kabla ya tarehe 25 Juni mwaka huu huku akisisitiza watumishi wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa weledi mkubwa ili kuepusha hoja zisizo na sababu.  

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri hiyo ambaye ni diwani wa kata ya Tutuo, Rashid Magope alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa watafanyia kazi maagizo yote aliyoyatoa katika kikao hicho ili kufikia malengo yao.

Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt Batilda Burian akiongea na madiwani na wataalamu wa halmashauri ya wilaya ya Sikonge kwenye kikao maalumu cha mapitio ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) jana katika ukumbi wa halmashauri hiyo. Picha na Allan Kitwe.