November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC Batilda aongoza wanatabora kumuombea Dua Hayati Mwinyi

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online,Tabora

MKUU wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Burian ameungana na viongozi na waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wakazi wa Mkoa huo kumuombea dua Rais Mstaafu wa awamu ya pili Hayati Ali Hassan Mwinyi aliyefariki dunia Februari 29,mwaka huu jijini Dar es salaam.

Akiongea katika ibada hiyo maalumu iliyoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Balozi Dkt. Batilda Burian ametoa salamu za pole kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuondokewa na kiongozi aliyetumikia taifa kwa mafanikio makubwa sana.

Amesema kuwa yeye binafsi na wakazi wote wa Mkoa huo watamkumbuka kwa mchango wake mkubwa wa kimaendeleo alioutoa kwa Mkoa huo na taifa kwa ujumla akiwa madarakani enzi za uhai wake.

Balozi Batilda ametaja baadhi ya alama zilizopo katika Mkoa huo ambazo ni kumbukumbu nzuri ya kazi yake kuwa ni uwepo wa shule za sekondari zilizopewa jina lake na uwanja wa kisasa wa mpira wa miguu wa Ali Hassan Mwinyi.

Ameongeza kuwa sifa nyingine za kipekee alizokuwa nazo Hayati Mwinyi na kumfanya awe kipenzi cha watu wengi kuwa ni ucheshi, mtu asiyependa makuu, mcha Mungu, mpole, mnyenyekevu, asiyependa dhuluma na mpenda maendeleo.

Shehe wa Mkoa wa Tabora Alhaj Ibrahimu Mavumbi amesema kuwa maisha ya Hayati Mwinyi yalikuwa hadithi nzuri na tamu miongoni mwa jamii kutokana na unyenyekevu wake mbele za Mwenyezi Mungu.

Awali Shekhe wa Wilaya ya Tabora Ramadhan Rashid amesema kuwa wakazi wa Mkoa huo na taifa kwa ujumla wamepoteza Kiongozi aliyekuwa ndani ya mioyo yao kutokana na utumishi wake mzuri, unyenyekevu, subira na msamaha, hivyo akatoa wito kwa viongozi wengine kuiga mfano huo.

Naye Kada wa Chama Cha Mapinduzi(CCM )na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mkoani hapa Said Ntahondi amesema kuwa atamkumbuka Hayati Mwinyi kwa kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini ikiwemo kuhamasisha jamii kufanya kazi kwa bidii, alifungua milango kwa wafanyabiashara kuagiza bidhaa kokote kule.

Amebainisha kuwa Hayati Mwinyi hakupenda uonevu kwa jamii anayoiongoza, alikuwa tayari kuwajibika mambo yalipoenda vibaya, alishawahi kumpa siku 3 Waziri wake ili wakulima wa tumbaku walipwe fedha zao.

Kwa upande wake Katibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Tabora Mohamed Abeid ametoa wito kwa jamii kuwapa malezi mema watoto wao ili kuenzi maisha mazuri ya Hayati Mzee Mwinyi.