Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Urambo
AKINAMAMA Mkoani Tabora wameadhimisha siku ya wanawake duniani kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo kuwezesha watoto 74 wanaolelewa katika Kituo cha Huruma Vision Center Wilayani Urambo kupata huduma ya Bima ya Afya.
Akiongoza harambee ya kuchangia watoto hao katika kilele cha maadhimisho hayo yaliyofanyika Kimkoa jana, Wilayani Urambo, Mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa huo Balozi Dkt Batilda Burian alifanikisha kukusanywa kiasi cha sh mil 4.4 ili kuwezesha watoto wote wanaolelewa katika kituo hicho kupata Bima ya Afya.
Alisema huduma hiyo ni muhimu sana kwani itamwezesha kila mtoto anayelelewa katika Kituo hicho kuwa na kadi ya matibabu ambayo itamsaidia kupata huduma za afya mahala popote atakapokuwa.
Alibainisha kuwa kila mtoto atalipiwa sh 50,400 kwa ajili ya kadi hiyo ambapo jumla ya sh 3,729,600/= zilihitajika, hivyo akinamama kutoka taasisi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wakachangia jumla ya sh 4,416,200.
Fedha taslimu zilizokusanywa ilikuwa sh 475,000 na kiasi cha sh mi 3.94 ni ahadi kutoka kwa akinamama mbalimbali, ambapo Mkuu wa Mkoa alimtaka kila aliyeahidi kukamilisha ahadi yake mapema iwezekanavyo ndani ya wiki hii.
‘Nawashukuru sana akinamama kwa moyo wa huruma na upendo mlioonesha, fedha hizi zitalipia Bima ya Afya kwa watoto 87, hivyo watoto wote 74 waliopo katika Kituo hiki watakapata bima na watakaongeza pia watapata’, alisema.
Awali akiongea katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa hamashauri ya Wilaya hiyo Baraka Zikatimu alisema watoto wanaolelewa hapo ni wale wanaotoka katika mazingira magumu, yatima na wenye albinism.
Aliongeza kuwa walianzisha kituo hicho kwa lengo la kusaidia watoto wote wasio na uwezo wakiwemo wanaozurura ovyo mitaani, wenye albinism na yatima kupata huduma stahiki za kijamii ikiwemo elimu, afya na malazi.
Alimshukuru Mkuu wa Mkoa, Viongozi wa Umoja wa Wanawake (UWT) na akinamama wote wa Mkoa huo kwa kuguswa na watoto hao na kuwachangia ili waweze kupata kadi za matibabu.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu