January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa maagizo kwa Machifu na Waganga wa Tiba asili wa mkoa wa Rukwa (hawapo pichani) katika kikao kifupi alichokutana nao ili kuwaelimisha juu ya ugonjwa wa Corona. (Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Rukwa)

RC awataka waganga wa tiba asili, machifu kuwa mfano kupambana na Corona

Na Mwandishi Wetu, Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza machifu pamoja na waganga wa tiba asili ndani ya mkoa wa Rukwa kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, kwa kuwa na ndoo za maji yanayotitirika na sabuni katika maeneo yao ya kazi ili kuwahamasisha na kuwaelimisha wateja wao wanaowapa huduma kuelewa umuhimu wa kunawa mikono ili kujikinga na ugonjwa huo.

Ameongeza kuwa haitakuwa na maana kama wamepata elimu halafu hawaitumii hali ambayo hakutakuwa na wa kumlaumu endapo ugonjwa huo utasambaa na kuangamiza watu, alisisitiza kuwa kutowaelimisha wateja wao na kushindwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo ni sawa na kulisaliti taifa, ikiwa serikali inaendelea kutimiza wajibu wake wa kutoa elimu ya ugonjwa huo kwa kutumia njia mbalimbali.

“Kwa upande wa maji mimi kwangu ni agizo, machifu wote muwe na ndoo ya maji tiririka na sabuni, muoneshe mfano, waganga wa tiba za asili, na nyinyi wote kwa umoja wenu mkawe na ndoo za maji tiririka na sabuni na elimu mmeipata vizuri, haitakuwa na maana kama mmepata elimu halafu kule mnakwenda hamuitumii halafu ugonjwa unakuja unatuangamiza, utamlaumu nani na elimu tumekupa, itabidi ujute kwamba wewe ni msaliti, umelisaliti taifa, umemsaliti na mungu pia,” alisema.

Mh. Wangabo ametoa maagizo hayo kwa nafasi yake kuwa kiongozi wa machifu mkoani Rukwa, katika kikao kifupi kilicholenga kutoa elimu ya ugonjwa wa Corona kwa machifu pamoja na viongozi wa waganga wa tiba asili wakiwemo wa Chama cha Waganga/ Wakunga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Mkoani Rukwa (CHAWATIRU).  

Aidha, Mh. Wangabo aliwataka machifu hao kukemea mila zinazowezesha kusambaa kwa ugonjwa wa Corona kwa haraka, ikiwemo watu zaidi ya mmoja kutumia chombo kimoja kunywa pombe za asili, familia kutumia chombo kimoja kutumbukiza mikono kwaajili ya kunawa, pamoja kutumia chombo kimoja cha kuchotea na kunywea maji katika mtungi.

Halikadhalika aliwataka waganga wa tiba asili kuwa na utatratibu wa kulipwa kwa kutumia huduma za mitandao ya simu ama benki ili kuepuka kushika fedha za wagonjwa ambao hawajulikani ugonjwa wao huku akisisitiza kutotowa dawa zinazopelekea mtu kupiga chafya kwa wingi jambo ambalo sio zuri hasa katika kipindi hiki cha mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa Corona.

Kwa upande wake, kaimu mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Emanuel Mtika aliwatahadharisha kuwa kuwatibu wagonjwa wa Corona ni gharama kubwa sana kiasi ambacho endapo ugonjwa huo utasambaa watu wengi wanaweza kupotea kwa kushindwa kufuata maelekezo ya wataalamu juu ya kujikinga na ugonjwa huo.

“ Kumtibu mgonjwa mmoja kwa siku ni shilingi milioni 48 na mgonjwa anatakiwa atibiwe kwa siku 15, je sisi huo uwezo tunao, hiki kitu kikitutokea huku sisi tutakwisha na ndio maana namshukuru mheshimiwa mkuu wa mkoa kwa kuona umuhimu wa kuitana ili tuelezane ukweli, hiki kitu kikitokea kwetu tutakwisha, kwahiyo nawaomba sana tutumie zile njia za kawaida za kupambana na hili janga,”Alisema.

Pia aliwataka waganga wa tiba asili pindi hasa wale wanaoishi katika mipaka ya Zambia na Kongo kuhakikisha wanapojiwa na mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa wa corona ni vyema wakamshauri au kumpeleka katika kituo cha afya kwa uchunguzi zaidi, au kuwasilisna na uongozi wa Kijiji kwa hatua zaidi.

Aidha, katika kukazia hilo afisa afya wa mkoa alishauri kuwa endapo mtu hana uwezo wa kununua ndoo ya maji tiririka kutokana na gharama yake anaweza kutumia kibuyu chirizi.