Na Bebi Kapenya
MKUU wa Mkoa wa Singida, Mhe Dkt. Binilith Mahenge amepongeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ujulikanao kama “TARURA e-Revenue Management Information System” (TeRMIS) katika Mkoa wa Singida.
Hayo yamejiri wakati wa kikao kazi kilicholenga kuwapatia mafunzo viongozi wa Mkoa wa Singida wakiwemo Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa juu ya Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ujulikanao kama “TeRMIS”.
Mkuu wa Mkoa ameeleza kuwa lengo la mfumo ni kuboresha ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatakayosaidia maendeleo na maboresho ya miundombinu ya barabara, pia mfumo unalenga kumpunguzia mtumiaji wa maegesho kero ya kudaiwa ushuru kwani mteja atalipa mwenyewe kwa kutumia mtandao wowote wa simu ya mkononi, au kupitia Tawi la Benki ya NMB na CRDB au kupitia kwa Mawakala.
“Nitumie fursa hii kuwapongeza TARURA kwa kuleta mfumo huu katika Mkoa wetu kwani mfumo utaleta tija katika ukusanyaji mapato ya Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi”, alisema Dkt. Mahenge.
Aidha, Dkt. Mahenge amewataka TARURA kuhakikisha elimu ya matumizi ya mfumo inafika kikamilifu kwa wananchi ili wawe na uelewa wa pamoja ili kuepusha malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi.
Pia, Mkuu wa Mkoa ametoa wito kwa wananchi kupokea mabadiliko hayo na kuanza kulipa wao wenyewe Ushuru wa Maegesho ili kuepuka adhabu na faini zisizo za lazima.
Kwaupande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Mhe. Juma Kilimbah ameipongeza TARURA kwa kuanza kutumia mfumo huo kwani mapato ya Serikali yataongezeka kwakuwa kwa kutumia mfumo huo unalipa moja kwa moja serikalini na mapato hayo yatasaidia kuboresha miundombinu ya barabara katika Manispaa ya Singida.
Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Mapato yaani “TARURA e-Revenue Management Information System” (TeRMIS) unaosimamiwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeanza kufanya kazi katika Mkoa wa Iringa na Singida na unatarajia kusambazwa nchi nzima.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu