January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

RC aagiza watoto kuchanjwa dhidi ya polio

Na Hadija Bagasha, TimesMajira online, Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Adam Malima ameitaka jamii kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano anachanjwa chanjo ya Polio ili kuondokana na madhara ya ugonjwa wa kupooza mwili.

Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa zoezi la chanjo ya polio kimkoa zoezi linalofanywa mara baada ya kuripotiwa mtu mmoja Nchini Malawi.

Akizindua kampeni hiyo mkuu wa mkoa wa Tanga Adam Malima katika kituo cha afya Duga aliwataka wazazi na walezi wote kuhamasika na kuelimishana wao kwa wao juu ya umuhimu wa chanjo hiyo kwa watoto ili kuweza kuwakinga na ugonjwa huo wa kupooza kwa viungo.

“Hii nguvu kubwa inayofanywa na Serikali itakuwa na maana na mafanikio makubwa sana kama nyinyi mkiipokea, katika hili wakina mama ninawaomba muwaangalie watoto wenu hasa katika ugonjwa huu tutahangaika baadaye kumbe tulishindwa kumpa chanjo hii kwa wakati , tuwape ujumbe na wenzetu nakuombeni sana tuwawahi mapema kabla hawajaathirika ” alisema Malima.

Mwakilishi wa shirika la Afya Duniani ‘WHO’ Faraja Lutambi alisema virus vya ugonjwa wa kupooza ambavyo husambaa kutoka kwao mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya hewa na maji au kwa kushikana mikono namna pekee ya kupambana na ugonjwa huo ni kwa kupitia chanjo ikiwa mpaka sasa hakuna matibabu ya Moja kwa moja mara mgonjwa anapogundulika.

“Tunakwenda kuwachanja watoto wetu tuweze kuwakinga kwa sababu ugonjwa huu umeibuka upya kuna ukaribu sana Kati ya Tanzania na Malawi , virus hivi vinaenea kwa njia ya kuambukizana kwa kushikana mikono, maji au chakula hivyo namna pekee ya kupambana na ugonjwa huu ni kwa njia ya chanjo ambao hauna tiba mpaka sasa hivi, kwa hiyo hatu lazima tuwakinge watoto wetu tusimsubiri kupata tatizo hili ni vizuri kama wazazi na walezi kuchukua hatua”alisema Dkt .Lutambi.

Mwakilishi wa wizara ya afya kutoka mpango wa taifa wa chanjo Immaculate Dotto akiwa Mkoani Tanga wakati wa uzinduzi wa chanjo hiyo iliyofanyika katika kituo cha afya Duga ambapo alisema kuwa ili kuhakikisha wanatimiza adhima ya serikali wanatarajia kuwafikia watoto wote nyumba kwa nyumba kuwapatia chanjo ikiwa ni kuchukuwa tahadhari dhidi ya ugonjwa huo .

Kampeni hiyo ambayo imenza jana jumatano nchi nzima kwa awamu ya pili , ilizinduliwa rasmi hivi karibuni mkoani Dodoma na waziri mkuu Kassimu Majaliwa ambapo tayari awamu ya kwanza ilishatolewa katika mikoa ya inayopakana na nchi ya Malawi ambayo ni Ruvuma Njombe, Mbeya na Songwe na inatarajia kuhitimishwa ifikapo may 21, 2022.

Akizungumzia kampeni hiyo ya kitaifa Immaculate alisema kuwa kwa wizara ya afya kwa kushirikiana na shirika la Afya Duniani ‘WHO’ wamekuwa wakifanya tafiti katika magonjwa mbalimbali ya mlipuko hapa nchini ambapo amebainisha kuwa katika tafiti hiyo hawakujagundulika mtoto yeyote aliyeathirika na ugonjwa huo.

“Kama wizara kwa kushirikiana na shirika la WHO tumekuwa tukifanya tafiti hususani ugonjwa wa polio kwa kuchukua sampuli kwa watoto na kufanyia vipimo katika maabara zetu na hata hivyo hatukufanikiwa kukutana na kesi yeyote , tunafanya kampeni hii kama tahadhari kwa nchi kutokana na mlipuko waliotokea Malawi sasa kutokana na muingiliano wa nchi hizi mbili tunalazimika kufanya kampeni hii na tunatarajia ifikapo tarehe 2may 2022 watoto wote tutakuwatumewafikia” alisema Immaculate.

Aidha kutokana na kampeni hiyo ya chanjo kufanyika nchi nzima ikipitia nyumba kwa nyumba aliwataka wazazi walezi na Tanzania kwa ujumla kutoa ushirikiano kwa waratibu na watakaosimamia utekelezaji wa zoezi hilo ili kufika malengo ya serikali kupitia wizara ya afya.

Akizungumzia takwimu za mkoa mganga mkuu wa mkoa wa Tanga Jonathan Budenu alisema kuwa wanatarajia kutoa chanjoa hiyo kwao watoto wapatao laki tatu na hamsini na nne elfu katika wilaya zote 8 na halamashauri 11 zilizopo.

“Tunawakinga watoto wetu pengine kama kuna ambao hawakumaliza na waliomaliza chanjo lakini tunawapongezea chanjo ili waweze kuwa na Kinga kamili hivyo zoezi hili linawahusisha viongozi wote wa serikali ngazi za wilaya halamashauri mitaa na vijiji wakiwemo watendaji kwa kushirikiana na wataalamu wa Afya hivyo ni vyema wananchi wakatoa ushirikiano ” alisema Budenu.

Aidha alisema kuwa tayari kuna timu tayari imeshapata mafunzo ya utekelezaji wa zoezi hilo ambapo amewataka wazazi walezi na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano ili kuweza kuwalinda na kuwakinga watoto dhidi ya ugonjwa huu wa Polio.

Kampeni hiyo ya kuwakinga watoto dhidi ugonjwa wa kupooza wa Polio ambayo inatekelezwa nchi nzima kwa awamu nne ikiwa sasa ni awamu ya pili linatarajiwa kuhitimishwa mwezi julay mwaka huu wa 2022.

Katika kufanikisha zoezi hilo Mkoa wa Tanga unatarajia kuchanja watoto wa umri chini ya miaka mitano wapatao laki tatu na nusu hadi mwezi july mwaka huu.

Zoezi hilo Kitaifa linatarajiwa kuchanja watoto zaidi ya milioni 10 na kwamba lengo ni kuimarisha kinga ya mwili huku malengo ya serikali yakiwa ni kuchanja watoto wote ndani ya mikoa 31.