December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Zanzibar Mohammed Raza Darams, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipotembelea ofisi za Majira na Mtandao wa TimesMajira, jijini Dar es Salaam leo.

Raza ashtukia mafisadi kujipenyeza Urais Zanzibar, ashauri wadhibitiwe

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

MFANYABIASHARA maarufu Zanzibar na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini kwa tiketi ya CCM, Mohammed Raza, amemuomba Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli, kuhakikisha vyombo vyake vya usalama vinawadhibiti mafisadi aliodai wamehamia Zanzibar na Dodoma ili kufanikiwa kumuweka madarakani Rais wa Zanzibar wanayemtaka.

Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Zanzibar Mohammed Raza Darams

Raza ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari alipotembelea chumba cha habari cha gazeti la Majira, na mtandao wa TimesMajira Online jijini Dar es Salaam jana.

Amesema, Zanzibar wana mchakato mzuri wa kidemokrasia ambapo hadi sasa wanaoomba kusimamishwa na CCM kuwania nafasi ya Urais wameishafikia 31.

Mwakilishi wa Jimbo la Uzini, Zanzibar Mohammed Raza Darams, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipotembelea ofisi za Majira na Mtandao wa TimesMajira, jijini Dar es Salaam leo.

Raza amesema Rais wa sasa Zanzibar, Dkt. Ali Mohammed Shein anamaliza muda wake na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idd, anastaafu baada ya kumaliza muda wake, hivyo alionesha wasiwasi wa mafisadi kutumia fursa hiyo kufanisha kumuweka madarakani Rais wa Zanzibar wanayemtaka.

Raza amemuomba Rais Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara) Philip Mangula na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally, kuwadhibi mafisadi hao ambao alidai kwa sasa wamehamia Zanzibar na wanapanga kuhamia Dodoma ili kumuweka Rais wa Zanzibar wanayemtaka.

Amesema hilo sio siri, kwani huko nyuma ilishawahi kujitokeza ndani ya CCM, ilikuwa hauwezi kuwa kiongozi kama hauna pesa au tajiri hajakudhamini.

“Nimekuwa kiongozi kwa miaka 32 na nimelelewa na CHAMA, Mzee Mwinyi (Ali Hassan) akiwa Mwenyekiti wa CCM aliunda kamati ya kukisaidia Chama, mimi kwa upande wa Zanzibar nilikuwa mjumbe, kwa hiyo naijua CCM,” amesema Raza.

Raza alisema, wakati huu ambapo wanaoomba kuwania Urais wa Zanzibar wamefikia 31, Mwenyezi Mungu ameishaweka mkono kwa mtu anayemtaka awe Rais.

“Rais ni mmoja na kamwe kundi halitaongoza chama, sasa nataka nimsaidie Rais wangu Magufuli awe na kikosi chake maalum cha vyombo vya usalama.

Na vyombo hivi vinasifika sana Afrika Mashariki nzima kwa kufanyakazi nzuri. Vyombo hivi vilifanyakazi nzuri mwaka 2015 Dodoma, tunataka kazi nzuri iliyofanyika mwaka 2015 huko Dodoma iendelezwe,” amesema Raza.

Alitoa mfano, akisema mwaka 1995 watu walikuwa wanadhani Msuya (Cleopa) angekuwa Rais, lakini Rais akaja kuwa Mkapa (Benjamin) na kwamba huko nyuma Salim (Salim Ahmed Salim) alikuwa anadhaniwa atakuja kuwa Rais, lakini Rais akaja kuwa Kikwete (Jakaya).

“Kwa hiyo ukija mwaka 2015, watu walitegemea Mzee Lowassa (Edward) na Membe (Bernard) watakuja kuwa Rais, lakini Rais akaja kuwa Magufuli, lakini kwa Zanzibar hakuna asiyejua kwamba Dkt. Bilal (Garib) alitabiriwa kuwa Rais, Rais akawa Dkt. Shein.

Huu ndiyo ukweli, kwa hiyo lazima Chama kitafute kiongozi mwenye uchungu na chama, mwenye uchungu na nchi, kuanzia ngazi ya wabunge, wawakilishi. Vivyo hivyo kwa upande wa wabunge na wawakilishi, wengi watapepesuka, kwa sababu walipoingia mwaka 2015 hawakutegemea Rais Magufuli atakuwa Rais,” amesema Raza.

Raza amesema wengi waliingia kwenye Baraza la Wawakili na Bungeni kwamba wameishapata dili.

Amempongeza Rais Dkt. Shein akisema amemaliza muda wake wa uongozi akiwa amefanyakazi yake vizuri na hakuwa mbaguzi wa rangi, hivyo anakwenda kupumzika vizuri. Hata hivyo alisema kuna baadhi ya watendaji wamefanya ufisadi, hao watashughulikiwa baadaye.

Aliwataka wabunge na wawakilishi wanapochukua fomu za kuwania uongozi wahakikishe hawana madeni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na hawana madeni kwenye taasisi zingine.

Lakini pia wahakikishe hawajachukua mikopo ya mamilioni ili ije kuwa kificho kwa CCM. Alisema kila kiongozi lazima atazamwe, kama anadaiwa na TRA au taasisi nyingine, aangaliwe kama amewatumikia wananchi,” alisema.

Alisema vigezo hivyo vikiangaliwa anaamini wabunge wengi wataacha wenyewe. “Dalili ya mvua ni mawingu, mafisadi wameishaanza kupiga hodi, wakiachiwa maana na hata Muungano utatetereka.

Ushindani Zanzibar

Akizungumzia ushindani wa kisiasa Zanzibar, Raza alisema kwa sasa upo kwa vyama viwili vya CCM na ACT-Wazalendo. “Kwa sababu ACT-Wazalendo ndiyo ile iliyokuwa CUF. Wanasema ulipo tupo, Zanzibar majimbo yatakuwa ya CCM na ACT-Wazalendo, japo vyama vingine vitashiriki, lakini haviwezi kupata jimbo,” amesema Raza na kuongeza;

“Kama ACT-Wazalendo itashiriki uchaguzi Serikali ya Umoja wa Kitaifa hauwezi kuiepuka, lakini la pili Zanzibar ushindani ni wa kihistoria, hivyo tuhakikishe tunapata wawakilishi wenye sifa, siyo kusema huyo nilisoma naye, tunawataka watu wanaoenda kushindana.

Baraza linalokuja sio kama hili lililopita, linalokuja tunakwenda kushinda kwa hoja,” alisema. Alisema suala la usalama wa Zanzibar ni suala la kipaumbele cha kwanza. Alisisitiza wanataka kiongozi anayekuja ajue usalama wao ni Muungano na CCM.

Uongozi wa Rais Magufuli

Akizungumza uongozi wa Rais Magufuli, Raza amesema amefanyakazi nzuri akiwa amewekeza sana kwa wanyonge, wafanyakazi na wakulima. Alisema huko nyuma watu walikuwa wakifanyakazi kwa mazoea hata maadili yalipotea kwa wafanyakazi.

“Wafanyakazi na mafisadi wachache waliodhi Tanzania na Zanzibar, kwa kusema wao ndiyo wenye maamuzi, lakini leo tumefikia sehemu Mungu ametuletea Rais ambaye ameonesha mfano katika Ardhi ya Tanzania,” alisema Raza na kuongeza;

“Heshima ya Tanzania imerudi duniani kote, kila mmoja anauliza Rais Magufuli ni nani? Lakini nashukuru ameturejeshea heshama, kubwa ninachomuomba Mwenyezi Mungu amrejeshe Ikulu,” amesema Raza.