November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ratiba na mwongozo taasisi zinazohamia Dodoma yakamilika

Na Zena Mohamed,TimesmajiraOnline,Dodoma.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene amesema kuwa Serikali imekamilisha ratiba na mwongozo utakaowezesha Taasisi za Serikali ambazo bado zinaendelea kutekeleza majukumu yake Dar es Salaam kuweza kuhamishia shughuli zao Jijini Dodoma kwa awamu.

Simbachawene amesema hayo Jijini hapa leo,Januari,16,2023,wakati wa hafla ya  kukabidhi vibali vya ujenzi wa ofisi za taasisi Dodoma ambapo muongozo huo umeelekeza 42 kuhamia Dodoma ndani ya mwaka huu wa fedha huku taasisi nyingine  36 zitahamia Dodoma katika mwaka ujao wa fedha.

Katika hatua nyingine Simbachawene amesema  taasisi 19 zitahamia katika mwaka fedha  2024/25 wakati taasisi 27 zimeelekezwa, kwa kuzingatia aina ya majukumu zilizonazo, kuendelea kutekeleza majukumu yake Mkoani Dar es Salaam.

“Serikali ilikuwa na jumla ya taasisi 189 zilizokuwa zinatekeleza majukumu yake Jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, kutokana na zoezi la Serikali kuhamishia shughuli zake Jijini Dodoma,  taasisi 55 za serikali zimetekeleza maelekezo hayo kwa kuamua kujenga ofisi zake Dodoma,

“Hadi sasa taasisi 20 zimekamilisha ujenzi, taasisi 16 zinaendelea na hatua mbalimbali za ujenzi, taasisi nyingine 19 zipo katika maandalizi ya kuanza ujenzi baada ya kupata vibali vya ujenzi kutoka kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,”amesema.

Vilevile,Simbachawene ametoa maagizo manne kwa Taasisi hizo  ili kuimarisha mpango huo wa Serikali kuhamishia taasisi zake Dodoam, ambapo moja ni Taasisi zote zinazoendelea na ujenzi Dodoma zihakikishe ujenzi huo unakamilika kwa kuzingatia taratibu zote za ujenzi ikiwemo ubora, muda, bajeti iliyotengwa na thamani ya fedha ili kuleta tija inayotarajiwa.

Mbili ni Taasisi zote zilizoelekezwa kuhamia Dodoma kwa mujibu wa ratiba niliyoitoa leo zihakikishe zinatekeleza maagizo hayo na Makatibu Wakuu wa Wizara husika wahakikishe wanasimamia mpango kazi wa utekelezaji wake.

Tatu ni Ofisi ya Katibu Mkuu  Sera, Bunge na Uratibu kwa kushirikiana na Mamlaka husika iendelee kuratibu Mpango wa Serikali na Taasisi zake kuhamia Dodoma pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi na uboreshaji wa huduma mbalimbali za kijamii Dodoma.

Nne ni Taasisi nyingine ambazo bado hazijaanza maandalizi ya ujenzi Dodoma ziwasilishe Ofisi ya Waziri Mkuu mahitaji ya viwanja vya ujenzi wa Ofisi za Taasisi Dodoma kwa ajili ya uratibu wa pamoja

Aidha Simbachawene amebainisha kuwa majengo ya taasisi za serikali yanajengwa katika maeneo ya NCC Link, Medeli, Njedengwa Mtumba na Kikombo kwa kufuata mwongozo uliopo katika Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma.

Alisema ujenzi unaoendelea unategemewa kubadili mandhari ya Jiji la Dodoma pamoja na kupunguza changamoto ya ofisi na hivyo kuwezesha zoezi la serikali na taasisi zake kuhamia Dodoma kwa ufanisi zaidi. 

Kwa mujibu wa Simbachawene alisema serikali inaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa majengo ya kudumu ya ofisi 26 za wizara yanayojengwa katika awamu ya pili.
Aliafanua kuwa ujenzi huo umefikia wastani wa takriban asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika kabla ya Oktoba mwaka huu kwa gharama ya sh. bilioni 675.

“Serikali inaendelea kuchukua hatua mahsusi za uboreshaji wa miundombinu ya miradi ya kimkakati Dodoma ikiwemo ujenzi wa uwanja Ndege Msalato utakaogharimu sh. billioni 165 ambao ujenzi wake umefikia asiimia 11, ujenzi wa barabara za mzunguko zenye urefu wa kilometa 112 na utagharimu sh. bilioni 221 ambao ujenzi umefikia asilimia 20, ujenzi wa Bwawa la Farkwa ambalo litazalisha maji mita za ujazo 130,000 kwa siku na kugharimu sh. bilioni 325.

Aliongeza kuwa”Serikali inaendelea na  ujenzi wa mtandao wa maji kutoka Bwawa la Mtera hadi Dodoma utakaozalisha mita za ujazo 128,000 kwa siku, uboreshaji wa barabara za mtandao wa lami katika Jiji la Dodoma na ujenzi wa reli itakayozunguka Jiji la Dodoma ili kurahisisha huduma za usafirishaji na kupunguza msongamano.

Simbachawene alizitaka sekta binafsi kuendelea kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa makao makuu katika maeneo mbalimbali ya utoaji wa huduma za kijamii .

Amezitaja huduma hizo kuwa ni shule na hospitali zenye hadhi ya kimataifa, hoteli za nyota tano, migahawa ya kisasa, kumbi zenye hadhi ya kimataifa, nyumba za kisasa za makazi, huduma za usafiri wa anga na ardhini, utalii, na maduka makubwa

Amekabidhi  vibali vya ujenzi wa ofisi za taasisi 20 za serikali kwa lengo la kutambua mchango wa katika uendelezaji wa makao makuu ya nchi kwa kuanza maandalizi ya ujenzi wa taasisi zao na kutoa vyeti vya pongezi kwa taasisi 35 zilizokamilisha na zinazoendelea na hatua mbalimbali za ujenzi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,Bunge na Uratibu ,Dkt.John Jingu amesema kuwa lengo la kukabidhi vibali vya ujenzi ni kuendeleza ujenzi kwa Taasisi mbalimbali hapa Dodoma.

Dkt.Jingu ametaja gharama za ujenzi huo kwa taasisi zilipewa vibali leo(jana) kuwa ni  bilioni 351 huku  jumla  ya gharama za ujenzi wa taasisi zote zilizopewa vibali  ni bilioni 875.