Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online
MECHI ya marudiano ya Ligi Mabingwa Afrika kati ya wenyeji Simba na FC Platinum sasa ni rasmi itachezwa saa 11:00 jioni badala ya 1:00 kama ilivyotangazwa awali.
Muda wa kuanza kwa mchezo huo umerudishwa nyuma baada ya uongozi wa klabu ya Simba kuandika barua kwenda Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuomba mchezo huo ubadilishwe muda kutokana na jografia ya mji wa Dar es Salaam ulivyo.
Akizungumza na Vyombo vya Habari, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Haji Manara amesema kuwa, baada ya kuandika barua kwenda CAF kuomba mchezo huo kuchezwa saa 11 jioni, Shirikisho hilo limeridhia na kuwapa majibu kuwa sasa mchezo huo utachezwa muda huo badala ya ya 1:00 usiku.
Amesema kuwa, kilichowasukuma kupeleka maombi hayo ni kutaka mashabiki wengi zaidi kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo kwani nguvu ya wachezaji wao ipo kwa mashabiki ambao siku zote wamekuwa na msukumo wa kikosi chao kupata matokeo mazuri katika uwanja wao wa nyumbani.
“Klabu ya Simba mtaji wake ni mashabiki na ndio mtakaotupa matokeo siku ya mchezo wetu wa marudiano, nguvu ya mashabiki imepelekea klabu zote kubwa za Afrika kushindwa kutamba hivyo ikiwa tutajitokeza kwa wingi, ndani ya dakika 20 tutakuwa tumeshamaliza mchezo ,”.
“Lakini pia ikiwa tutafuzu basi kizazi hiki cha kina Clatous Chama, Aishi Manula, John Bocco na wengine kitakuwa bora kwani kitakuwa ni kizazi cha kwanza kwenda kufuzu kucheza hatua ya makundi ya Ligi Mabingwa mara ya pili, ni niwahakikishie kwa jinsi morali ilivyo basi ni wazi kazi itakuwa nyepesi kwetu, ” amesema Manara.
More Stories
Zanzibar kuzalisha wachezaji wenye vipaji
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania