January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rasmi Mwamnyeto mali ya Yanga

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

HATIMAYE baada za sarakasi za muda mrefu, Yanga imenasa saini ya beki wa Coastal Union ya Tanga aliyesaini kandarasi ya miaka miwili kuitumikia timu hiyo.

Usajili huo sasa unazima tetesi za muda mrefu zilizokuwa zikimuhusisha beki huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kujiunga na Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) Simba kwa dau alilolihitaji la milioni 80.

Awali baadhi ya wadau wa soka hapa nchini walikuwa wakiipa nafasi kubwa Simba kunasa saini ya beki huyo na wapo waliodai kuwa kwa asilimia zaidi ya 80 alikuwa amemalizana na Simba na alichokuwa akisubiri ni kumalizika kwa msimu.

Lakini siku chache baada ya kauli hiyo, meneja wake aliweka wazi kuwa, licha ya Simba kumuhitaji lakini Yanga ndio waliokubali dau walilolihitaji hivyo kulikuwa na uwezekano mkubwa akajiunga nao kwa ajili ya msimu ujao.

Wakati wa tetesi hizo, Mwamnyeto aliwahi kuuambia Mtandao huu kuwa, mipango yake ilikuwa ni kuitumikia moja ya klabu hizo mbili mbili zenye ushindani mkubwa lakini tayari alikuwa ameshafanya maamuzi atasaini klabu ipi.

Mbali na Mwamnyeto, timu hiyo pia imemsajili beki wa kushoto, Yassin Mustapha kutoka Polisi Tanzania kwa mkataba wa miaka miwili kama ilivyo kwa Mwamnyeto.

Usajili huo unaonesha wazi kuwa Yanga imenza kuimarisha kwanza safu yao ya ulinzi na hadi sasa imefikisha usajili wa wachezaji watatu wapya baada ya juzi kumsajili kiungo Zawadi Mauya.