January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rasmi Julian Nagelsmann kocha mpya Bayern Munich

MUNICH, Ujerumani

ALIYEKUWA kocha wa RB Leipzig inayoshiriki Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga) Julian Nagelsmann, amejiunga na mabingwa watetezi wa Ligi hiyo Bayern Munich kwa kandarasi ya miaka mitano.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Bayern Munich zimesema, Kocha wa sasa, Hansi Flick alikuwa ametangaza nia yake ya kuondoka katika kikosi Cha The Bavaria. Flick amehusishwa sana na kazi ya kuinoa timu ya taifa ya Ujerumani kuchukua mikoba ya Joachim Low ambaye anatarajia kujiuzulu baada ya msimu huu wa Mashindano ya EURO.

Nagelsmann, mwenye umri wa miaka 33 raia wa Ujerumani ni mmoja wa mameneja wenye Umri mdogo waliopo Katika viwango vya juu huko Ulaya na aliiongoza Leipzig kutinga nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka jana.

Mjerumani huyo anatarajiwa kuigharimu Bayern zaidi ya pauni milioni 20 kwa fidia sehemu iliyobakia Katika Mkataba wake Huko Leipzig. Nagelsmann atakuwa Kocha wa Bayern Munich msimu ujao kuchukua nafasi ya Hansi Flick.

“FC Bayern ilikubali ombi la kocha mkuu wa sasa Hansi Flick kutaka mkataba wake umalizwe tarehe 30 Juni 2021, miaka miwili mapema kuliko tarehe ya mwisho ya kumalizika,” imesema taarifa kutoka Bayern Munich.