January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria

Rais wa Nigeria aagiza maelfu ya wafungwa waachiwe

ABUJA, Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria amemtaka Jaji Mkuu wa nchi hiyo, Ibrahim Tanko Muhammad awaachilie huru wafungwa ambao wamekuwa wakisubiri kusikilizwa kesi zao kwa kwa muda wa miezi sita sasa au zaidi.

Hatua hiyo inatajwa kuwa moja ya njia ya kukabiliana na ueneaji wa virusi vya Corona (COVID-19) katika Taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika.

Rais Buhari alinukuliwa akisema kuwa, asilimia 42 ya wafungwa 74,000 wamekuwa wakisubiri kusikilizwa kesi zao, hivyo Jaji Mkuu awaachilie huru wafungwa hao.

Pia alieleza katika agizo lake hilo kwamba, msamaha huo utawahusu wafungwa wanaokabiliwa na kesi ambazo sio za jinai, wenye umri mkubwa na wanaogua maradhi mbalimbali.

Agizo hilo linajiri wiki mbili tu baada ya agizo jingine kama hilo ambapo Rais Buhari alitaka kuachiliwa huru wafungwa 2,600 wenye umri wa miaka 60 na zaidi.

Miongoni mwao ni wanaogua maradhi hatari na wale ambao wamebakiza miezi sita tu kabla ya kumaliza vifungo vyao na ambao kimsingi walihukumiwa adhabu ya kwenda jela miaka mitatu au zaidi.

Wakati huo huo, hivi karibuni Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) ilitoa wito wa kuachiwa huru kiongozi wake, Sheikh Ibrahim Zakzaky anayekabiliwa na hatari ya kuambukizwa virusi vya corona akiwa kizuizini, takwa ambalo hata hivyo bado halijatekelezwa na Serikali.

Wachambuzi wa masuala ya kijamii wanabainisha hayo yanajiri, licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kuwahi kutoa hukumu iliyosisitiza kuwa Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe hawana hatia yoyote na ikaamuru waachiliwe huru, lakini wawili hao bado wameendelea kuwekwa jela licha ya hali zao za afya kuwa mbaya.

Ni tangu walipotiwa hatiani mwaka 2015 baada ya jeshi la Nigeria kushambulia Husseiniya ya Baqiyatullah katika mji wa Zaria huko Kaduna.

HATUA

Mbali na hayo Harakati ya An Nahdhah ya Tunisia imetangaza kuwa, zaidi ya vyama 200 duniani vimesaini taarifa kwa lengo la kushrikiana katika mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Harakati ya An Nahdhah ya Tunisia imeeleza kuwa, harakati hiyo pamoja na vyama zaidi ya 200 kote duniani vikiwemo chama tawala cha Afrika Kusini cha African National Congress (ANC), Chama cha Uadilifu na Ustawi cha Uturuki na Chama cha Umoja cha Urusi vimesisistiza katika taarifa yao ya pamoja juu ya kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na virusi vya corona.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya An Nahdhah, vyama hivyo vimeazimia kwa dhati kukabiliana na virusi vya corona katika wakati huu.

Vyama hivyo zaidi ya 200 kote duniani pia vimezitolea wito nchi zote duniani kutoa kipaumbele kwa suala la usalama na afya ya wananchi wao na kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na maambukizi ya corona.

Vyama vikuu katika nchi mbalimbali duniani vimesisitiza kuwa, vinaunga mkono kuboreshwa ubadilishanaji wa taarifa kuhusu mapambano dhidi ya virusi vya corona na kushirikiana katika sekta ya tiba ikiwemo kushauriana kwa pamoja ili kufanikisha utengenezajiwa dawa na chanjo dhidi ya virusi vya corona.

Sambamba na kutoa huduma za kiufundi na kifedha kwa nchi zinazohitaji ili kuhakikisha ugonjwa huo unatokomezwa.