Ibrahim Boubacar Keïta ambaye ni Rais wa Mali amejiuzulu muda mfupi baada ya kuwekwa kizuizini na Jeshi la nchi hiyo .
Akilihutubia taifa kwa njia ya televisheni, Bwana Keïta amesema anaivunja serikali na bunge.
”Sitaki damu imwagike ili mimi kuendelea kubaki madarakani,” aliongeza.
Hatua hii imekuja saa kadhaa baada ya kiongozi huyo wa juu na Waziri Mkuu Boubou Cissé kupelekwa kwenye kambi ya jeshi karibu na mji mkuu Bamako, hatua iliyosababisha mataifa ya Afrika Magharibi na Ufaransa kulaani kitendo hicho.
”Ikiwa leo, sehemu ya vikosi vilivyo na silaha wanataka hili liishe kwa kuingilia kati, nina cha kufanya?” alisema Keïta.
Rais huyo pamoja na waziri mkuu wake walikamwatwa na jeshi baada ya maandamano yaliyodumu kwa miezi kadhaa kumtaka bwana Keita kung’atuka madarakani.
Keita ambaye alikua katika muhula wake wa pili wa uongozi alikua akituhumiwa kusababisha mdororo wa kiuchumi nchini humo pamoja na kushindwa kuyazuia makundi ya wapiganaji wa kiislamu ambayo yameharibu amani ya nchi hiyo.
Awali msemaji wa serikali ya Mali aliiambia BBC kwamba Rais wa nchi hiyo pamoja na Waziri Mkuu wamekamatwa na jeshi.
Yaya Sangaré ambaye ni msemaji wa serikali amesema Rais Ibrahim Boubakar Keita na waziri mkuu Boubou Cisse wapo katika mikono ya jeshi la nchi hiyo.
Hii inatajwa kwamba ni muendelezo wa kile kilichoanza kama maandamano ambayo yamedumu kwa miezi kadhaa sasa kupinga utawala wa Keita anayeshutumiwa kuisababishia nchi mdororo wa kiuchumi.
Wachambuzi wa masuala ya siasa tiyari wamelitaja tukio hili kuwa ni la mapinduzi.
Kukamatwa kwake kumewafurahisha maelfu ya waandamanaji ambao wamekua mitaani kila uchao kupinga utawala wake.
Katika maandamano mengine makubwa ya mwaka 2012, wapiganaji wa kiislam walilichukua eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo huku kukiendelea kuwa na ukosefu wa amani na kushuhudiwa mapigano baina ya jeshi na vikosi vya wapiganaji wa kiislam katika maeneo kadhaa nchini humo.
More Stories
Elon Musk : Bill Gates atafilisika endapo…
Jay-Z aunganishwa na P Diddy kwa kumdhalilisha binti wa miaka 13
Samia avuna makubwa Mikutano ya Uwili G20