May 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais wa Finland afurahishwa na uhifadhi wa historia nchini

Na Mwandishi wetu,TimesmajiraOnline,Dar

RAIS wa Jamhuri ya Finland Alexander Stubb ameonesha kufuraishwa na uhifadhi wa historia uliopo katika makumbusho ya Taifa Jijini Dar es salaam huku akisema amejifunza na ametambua asili yake.

Pia Rais Stubb ametoa zawadi ya picha inayoonesha mashirikiano kati ya Tanzania na Finland tangu yalivyoanza.

Rais Stubb ametembelea Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es salaam mapema leo Mei 15, 2025 akiogozwa na Waziri wa Maliasiri na utalii, Balozi Dkt Pindi Chana na Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmoud Kombo Pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi

Katika ziara hiyo Rais Stubb amepata fursa ya kuangalia historia ya mwanadamu pamoja na kuona vifaa vya miaka ya nyuma vilivyokuwa vikitumiwa na mababu na mabibi.

Akizungumza na waandishi wa habari Rais Stubb amesema mashirikiano ya kihistoria kati ya Tanzania na Finland yalianza tangu nchi hizo zilipopata uhuru mwaka 1917 na Tanzania miaka ya 1960.

Amesema uhusiano huo wa kihistoria ulianza tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, pamoja na Rais wa kwanza wa Finland.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema kuwa ujio wa Rais Stubb ni matokeo ya uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Rais Stubb ameona fuvu la Zinjanthropus, zana za jadi, na hatua mbalimbali za maendeleo ya mwanadamu. Hili ni jambo la heshima kubwa kwa taifa letu,” amesema Chana.

Amesema kuwa kupitia ziara hiyo, Tanzania na Finland zimekubaliana kuendeleza mashirikiano katika maeneo ya mafunzo, tafiti za pamoja, na kubadilishana uzoefu katika sekta ya makumbusho na malikale.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Noel Luoga, amesema kuwa ziara hiyo imekuwa chachu na hamasa kubwa kwa taasisi hiyo kuendelea kutangaza utalii wa malikale.

“Tunatarajia kushirikiana na Finland katika tafiti, kuboresha maonesho kwa kutumia teknolojia za kisasa, pamoja na kuhakikisha makumbusho yanafika kwa jamii,” amesema Luoga.