Na Mwandishi Maalum, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapainduzi, Dkt. Ali Mohamed Shen amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Pemba, kufanya kazi kwa bidii na kuongeza kasi na ari ya utendaji kwani ofisi hiyo ina heshima ya pekee.
Rais Shein ameyasema hayo katika uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi iliyopo Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba iliyokwenda sambamba na uzinduzi wa nyumba za Ikulu huko Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba na kuwataka wafanyakazi wa ofisi hiyo kuendelea kulinda hadhi na heshima ya ofisi hiyo pamoja na kuendelea kushirikiana huku akisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwawekea mazingira mazuri ya kazi wafanyakazi wake wote.
Amesema kuwa, nyumba za eneo hilo la Ikulu zilikuwa zimechakaa sana na ndipo ndani ya miaka kumi iliyopita ofisi hiyo ilianza kazi ya kuzifanyia ukarabati na nyengine kuzijenga upya.
“Natoa pongezi kwa uongozi wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ukiongozwa na Waziri Issa Haji Gavu kwa kusimamia vizuri kazi za ujenzi wa jengo hilo hadi kukamilika na jana kuzinduliwa pamoja na wakandarasi wazalendo na Msanifu wa Majengo ambaye pia ni Meneja wa Majengo Ikulu Mohamed Abdulrahman Machungwa pamoja na Ramadhan Mussa Bakari ambaye ni Mkurugenzi wa Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA) ambayo ndio iliyojenga jengo hili,” amesema Rais Shein.
Kwa upande wa Pemba ofisi hiyo imefanya kazi kubwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha Ikulu ya Mkoani, kujenga Ikulu ya Micheweni pamoja na nyumba za Ikulu za eneo hilo na jengo hilo jipya la ofisi lililozinduliwa.
Amesisitiza kuwa, majengo yote hayo yamejengwa kwa fedha za Serikali pamoja na yale yote aliyoyazindua hivi karibuni zikiwemo nyumba za Kwahani, Maduka ya biashara Michenzani, nyumba za Mbweni pamoja na ofisi kadhaa za Serikali zikiwemo zile za Gombani Pemba.
Amesema kuna haja ya kutunzwa kwa jengo hilo ili liweze kutumika kwa muda mrefu na kuwataka wafanyakazi waharakishe kuhamia ili kuanza kazi huku akisisitiza kuwa thamani mpya zitaingizwa hapo baadae na hivi sasa watumie walizonazo.
Lengo la kujenga ofisi mpya na nzuri ni kwa ajili ya kuwapatia wafanyakazi maeneo mazuri ya kufanya kazi na kuwaweka katika mazingira bora ya kazi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.
Amesema kuwa, hatua hiyo itawapelekea wafanyakazi kuridhika kwani iwapo wafanyakazi wataridhika ndipo wataweza kufanya kazi vyema ya kuyatunza na kuyalinda mazingira na kueleza kwamba kila mmoja ana jukumu la kulitunza na kulienzi jengo hilo na kutaka majengo yote ya Ikulu yaendelezwe na yatunzwe.
Amesema, azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuanzisha Wakala wa Nyumba na Majenzi, Shirika la Nyumba pamoja na kuanzisha Kampuni ya Majenzi ya Serikali ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza gharama za ujenzi kwa majengo ya Serikali.
Amesema kuwa, uzoefu wa Serikali kujenga majengo yake wenyewe unatokana na uzoefu wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Mzee Abeid Amani karume ambapo katika uongozi wake majengo mengi yalijengwa kwa gharama za Serikali.
Ametumia fursa hiyo kuwaongeza wafanyakazi wote wa Ofisi ya Rais wa Unguja na Pemba pamoja na wale wote waliowahi kufanya kazi katika ofisi hiyo na hivi sasa wamehamishiwa ofisi nyingine.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Ussi Gavu alitoa shukurani kwa Rais Dkt.Shein kwa maelekezo yake mbalimbali pamoja na miongozo yake katika kuhakikisha ujenzi unafanyika vyema katika majengo yote ya Ikulu za Pemba, Unguja, Dar es Salaam na Dodoma.
Waziri huyo ametoa shukurani kwa mashirikiano makubwa yaliyofanyika katika ujenzi huo na kumpongeza Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi kwa ushrikiano wake pamoja na Maafisa Wadhamini wote walioshiriki.
Mapema Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Salum Maulid Salum alitoa shukurani kwa Rais Dkt. Shein kwa kutia shime ya kujienga jengo hilo na kulimaliza kwa wakati.
Maamuzi ya ujenzi wa jengo hilo yanaenda sambamba na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015-2020.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â