January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia:Watu 13 wamepoteza maisha Kariakoo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,amesema hadi kufikia saa nne asubuhi,Novemba 17,2024,jumla ya watu 84 waliokolewa na kufikishwa hospitali kupatiwa matibabu, kati ya hao mejeruhi 26 bado wanaendelea na matibabu.Huku 13 wamepoteza maisha katika tukio la kuporomoka kwa jengo la gorofa eneo la Kariakoo jijini Dar-es-Salaam.

Dkt. Samia,amesema hayo Novemba 17,2024, wakati akitoa salamu za pole,jijini Rio de Janeiro nchini Brazil,ambapo yupo kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi Wanachama wa Kundi la G20 unaotarajiwa kuanza,18 Novemba, 2024.

Amesema serikali itabeba gharama za matibabu kwa wote waliojeruhiwa na kuhakikisha waliofariki wanasitiriwa ipasavyo

Huku akieleza kuwa hadi sasa sababu za kitaalamu za jengo hilo kuporomoka bado hazijachunguzwa na kubainishwa,kwani kipaumbele kwa sasa ni kuwaokoa wananchi waliokua ndani ya jengo hilo.

Pia amemtaka Waziri Mkuu,kuongeza timu ya wakaguzi majengo,waendelee na zoezi la kukagua eneo lote la kariakoo na kupata taarifa kamili ya hali ya majengo ilivyo.

Pia amelitaka jeshi la polisi kupata taarifa kamili kutoka kwa mmiliki wa jengo lililoporomoka, jinsi ujenzi ulivyokuwa ukifanyika.

Hata hivyo Dkt. Samia ametoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki walioguswa na tukio hilo,huku akiwaomba Watanzania,kuwaweka kwenye maombi watu wote
Walioathirika na tukio hilo na kuwaombea pumziko la amani wote waliotangulia mbele za haki.

“Serikali itaendelea kutoa taarifa zaidi kuhusu zoezi la uokozi hadi hapo zoezi hili litakapokamilika,”.

Vilevile,amevishukuru vyombo vyote vya usalama ambavyo vinaendelea na zoezi hilo la uokoaji wa watu,mashirika binafsi na wananchi waliotoa ushirikiano katika zoezi hilo pamoja madaktari wanaoendelea kuwahudumia majeruhi.

Kadhalika,amesema serikali inahakikisha taarifa za uchunguzi zitakaopatikana pamoja na hatua zitakazochukuliwa zitaekwa wazi kwa wananchi.