December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia:Kuhamishia Makao makao makuu Dodoma ni jitihadi za awamu zote za uongozi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu ameeleza historia ya uamuzi wa kuhamisha makao makuu ya nchi Dodoma, ambapo amesema uamuzi huo umekamilika kutokana na jitihada za awamu zote za uongozi wa nchi.

Rais Samia amesema hayo jijini hapa leo,Mei 20,2023 wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo jipya la Ikulu Chamwino,Dodoma ambayo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kitaifa pamoja na wastaafu wa awamu zilizopita.

Amesema kuwa mchakato wa kuhamishia makao makuu Dodoma ulianza muda mrefu na ulipita katika ngazi mbalimbali za chama na baadaye kutangazwa ambapo amesema historia inaeleza kwamba mwaka 1966, Joseph Nyerere, mdogo wake Mwalimu Nyerere, aliwasilisha hoja binafsi bungeni ya kutaka Dodoma iwe makao makuu ya nchi lakini hoja hiyo ilipingwa na wabunge.

“Pendekezo hilo liliwasilishwa pia ndani ya chama na mwalimu Nyerere akasema ili pendekezo hilo lipitishwe, sharti liungwe mkono wa matawi mengi nchi nzima,”amesema

Rais Samia amesema kuwa tangu mwaka 1973 Mwalimu Nyerere alipotangaza umma uamuzi kuufanya mji wa Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, kazi ya kuuendeleza mji huo ilianza ili kuufanya uwe na hadhi ya makao makuu ya Serikali.

azi hiyo haikuwa rahisi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kuifanya safari hiyo kuwa ndefu kuliko ilivyopangwa.

“Tangu mwaka 1973 hadi leo mwaka 2023, ni kama miaka 50 hivi badala ya miaka 10 na huu ni umri wa wengi mliomo humu ukumbini kazi hiyo haikuwa rahisi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kuifanya safari hii kuwa ndefu kuliko ilivyopangwa,

“Kazi ilikuwa ngumu na ilikuwa ni jukumu la kila awamu iliyoingia madarakani kuwezesha kuanza ujenzi wa vitu mbalimbali ili Dodoma ichukue sura ya kuwa makao makuu ya serikali niwapongeze sana viongozi wa awamu zote kwa jitihada hizi zilizochukuliwa,”amesema.

Aidha ameeleza kuwa Julai 23, 2016, Hayati Magufuli aliukumbusha mkutano mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),kuhusu uamuzi wa kuhamisha rasmi shughuli za serikali kutoka Dar es Salaam kuja Dodoma

“Hivyo msukumo huo ulipelekea utekelezaji wa miradi mbalimbali ndani ya jiji la Dodoma uliendelea kwa kasi zaidi ikiwemo ujenzi wa Ikulu ya Dodoma ikiwemo eneo hili liliongezwa kutoka ekari 66 hadi kufikia ekari 8,473 na ndipo ujenzi wa jengo hili jipya kuanza na hii leo tunalizindua,”amesema Rais Samia.

Vilevile ameeleza kuwa ujenzi wa Ikulu ya Dodoma ni mradi wa pili kuukamilisha kati ya ile niliyoipokea kutoka kwa Hayati John Magufuli, mradi wa kwanza kuukamilisha ulikuwa ni daraja la Tanzanite.

“Mtakumbuka mradi wa kwanza kukamilisha ilikuwa Daraja la Tanzanite, Dar es Salaam huu ni mradi wapili na Insha Allah Mungu anipe uwezo nikamilishe yote,nashukuru Mungu kunipa uwezo wa kuifanya kazi hii,”amesema Rais Samia.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa baada ya kukamilika kwa Ikulu hiyo wanatarajia kujenga jengo la kisasa (Samia Complex) ndani ya eneo hilo kubwa la Ikulu lenye Ekari 8473 blna tayari michoro ipo na kwasasa amesema wanahangaika kutafuta fedha ili ujenzi uanze.

“Eneo hili bado kunakazi ya kufanya na hatua inayofuata ni ujenzi wa jengo la kisasa ambalo wasaidizi wangu wameliita Samia Complex ambalo litakuwa na ukumbi wa mikutano wa watu 2000 mpaka 3000,nyumba za viongozi hasa majirani zetu wa EAC na SADC, kutakuwa na Zanzibar Lounge,East Africa Lounge, uwanja wa Golf,viwanja vya michezo,njia za ndege na sehemu za historia za viongozi wa Nchi zetu,”amesema Rais Samia.