January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia: Yanga endeleeni kuipeperusha bendera ya Tanzania

*Awatakia kila lakheri michezo ijayo

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

HONGERENI Yanga SC, ndio kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan baada ya klabu hiyo kuibuka na ushindi wa goli 3-1 dhidi ya TP Mazembe, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi.

Akitoa pongezi hizo kupitia mtandao wake wa kijamii mara baada ya ushindi wa Yanga, Rais Samia alisema; “Hongera kwa Klabu ya Yanga kwa ushindi dhidi ya TP Mazembe katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.”

“Nawatakia kila la kheri katika michezo iliyosalia kwenye mashindano haya. Endeleeni kutupa burudani na kufanya kazi njema ya kuipeperusha vyema bendera ya nchi yetu kimataifa,” alisema Rais Samia.

Mchezo huo uliofanyika katika Dimba la Benjamini Mkapa Jijini Dar es Salaam, Januari 4 mwaka huu, ulishuhudiwa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma.

Mwinjuma aliongozana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, ambao kwa pamoja walifurahishwa na ushindi wa Yanga dhidi ya TP Mazembe

Baada ya mchezo huo, Yanga ilikabidhiwa kiasi cha shilingi milioni 15 ikiwa ni zawadi ya goli la Mama, kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Sami kuhamasisha mchezo wa soka nchini.

Katika mchezo huo magoli ya Yanga SC, yalitiwa kimiani na mshambuliaji mzawa Clement Mzize ambaye alifanikiwa kushinda mabao mawili dakika 33 na 60, huku bao la tatu likifungwa na kiungo wa Kimataifa wa Burkina Faso Stephane Aziz Ki dakika ya 56.

Kwa ushindi huo Yanga SC imefikisha pointi nne na kusongea nafasi ya tatu na kuishusha TP Mazembe nafasi ya nne wakiwa na pointi mbili.

Al Hilal Omdurman inaendelea kuongoza kundi A wakiwa na pointi tisa, ikifuatiwa na MC Alger yenye pointi nne na wastani mzuri wa mabao zaidi ya Yanga SC baada ya wote kucheza mechi tatu.