September 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia: Tuwakatae wote wanaotaka kutugawa

*Asema sisi wote ni wamoja, ndugu, akemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili,
ataka kila mmoja akague boma lake, atamani matamasha hayo yawe ya kibiashara

Na Cresensia Kapinga, TimesmajiraonlineSongea

RAIS Samia Suluhu Hassata, amewataka Watanzania kuwakataa wote wanaotaka kuwagawa kwa sababu za kiasiasa au kiitikadi kwa sababu sisi wote ni wamoja na ni ndugu.

Rais Samia alitoa rai hiyo ikiwa ni siku yake ya kwanza ya ziara yake mkoani Ruvuma ambapo pia alifunga Tamasha la Tatu la Utamaduni ambalo lilihudhuriwa na machifu na wananchi kutoka makabila mbalimbali nchini.

“Watanzania tuwakatae watu wote wanaotaka kutugawa kwa sababu za kisiasa au kiitikadi, sisi sote ni wamoja,” alisema Rais Samia.

Kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Rais Samia alitoa wito kwa kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura asikubali kubaki nyumbani. Alisema uchaguzi ni sehemu ya utamaduni wa kisiasa, kwa hiyo aliwasihi Watanzania kuendelea kudumisha amani kabla,wakati na baada ya uchaguzi ili tuendelee kutunza utamaduni wetu.

Akizungumzia Tamasha la Utamaduni, Rais Samia alisema matamasha hayo ni kielelezo cha kuthamini na kuenzi utamaduni wetu. ” Kwa hiyo tumekusanyika kutoka kila pande ya nchi, hivyo misingi hiyo ilindwe na kuendelezwa,” alisema Rais Samia na kuongeza;

Madhumuni ya matamasha ya utamaduni ni kulinda utamaduni. Yanafungua fursa za kiuchumi kupitia fursa za kiutamaduni zetu pamoja na vyakula na mavazi. “Nimeona vitu mbalimbali vya kitamaduni ambavyo vimeoneshwa, nawapa moyo ikiwemo wadau kuona namna ya kufanya utamaduni kuwa biashara ili utuletee manufaa ya kiuchumi.”

Alisema ni vizuri matamasha yajayo yawe na ushirika mkubwa zikiwemo sekta binafsi na yakiandaliwa vizuri, mikoa inaweza kuwa inayagombania ili kuwa wenyeji wa matamasha hayo. Aliwataka wafanyabiasha mkoani Songea kufungua hoteli kwa sababu biashara zinakuwepo.

Alitolea mfano kwamba zaidi wa watu 16,000 wanaowasili Ruvuma kwa ndege kwa siku tatu kwa wiki, akisema hiyo ni fursa nzuri na kielelezo cha mkoa huo kufunguka kiuchumi.

Rais Samia alieleza wazi kuridhishwa na upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Songea. Rais Samia alisema atakuwa mkoani humo kwa kazi mbalimbali, ambapo jana jioni alikutana na wazee.

Kazi zingine atakazozifanya ni kuzungumza na wananchi na kukagua miradi mbalimbali, kwani Serikali imepeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ya kukuza uchumi.

“Katika ziara yangu nitakagua miradi ambayo imekuwa ikitekelezwa na kufungua iliyokamilika , ambapo nimeanza na Uwanja wa Ndege wa Songea ambao nimeridhishwa sana na kazi iliyofanyika,” alisema na kuongeza kwamba mkoa huo unaenda kuwa kitovu cha biashara.

Kwa upande wa Kiswahili, Rais Samia alisema; “Hatuwezi kuenzi utamaduni wetu bila kuvutia lugha yetu, hivyo Wizara imepanga kufungua vituo 100 vya kufundisha kiswahili duniani kote kwa kushirikiana na Diaspora, hivyo alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia fursa hiyo.”

Alitoa wito kwa mitandao akitaka itumike kufundisha kiswahili ili kiendelee. Alisema vyuo vikuu vina nafasi ya kukuza kiswahili kwa kushirikiana na vyuo rafiki. Alisema kutokana na muingiliano wa maadili tumeanza kushuhudia mmonyoko wa maadili, vitendo hivyo vinaanzia nyumbani, hivyo alitoa rai kwa kila Mtanzania kukagua boma lake.”

Alisema kwa kushirikiana na machifu, na viongozi wa dini tushirikiane kusimamia maadili yetu.