Na Jackline Martin, TimesMajira Online
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufanya mkutano na vijana atakaowahutubia kisha kupokea taarifa ya namna ambavyo vijana wa Afrika wanajihusisha na kilimo na namna wanavyotumia fursa mbalimbali za kilimo
Pia Rais Samia atatoa hotuba yake ya namna ambavyo anaona ni muelekeo sahihi kwa Bara la Afrika wa kusaidia eneo la vijana kupata ajira kupitia kilimo
Hayo yamesemwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) kwa mwaka 2023 ambapo amesema mkutano huo utafanyika hapo kesho.
Msigwa amesema baada ya mkutano wa vijana, marais wote kutoka nchi mbalimbali ambao wamethibitisha kushiriki mkutano wa AGRIF watakutana na kufanya majadiliano kisha kutoa hotuba yao, lakini pia kupokea taarifa mbalimbali na kusoma maadhimio ya mkutano
Msigwa amesema mpaka sasa Marais ambao wamethibitisha kushiriki katika mkutano wa AGRF ni saba na wengine wanaweza kuongezeka au wakaja kuwakilisha .
Mbali na hayo, Msigwa amesema kesho Rais Dkt. Samia amewaalika wageni mbalimbali watakaokwenda Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya chakula cha jioni ambako huko kutatolewa tuzo ya Chakula Afrika
“Ni tukio muhimu la kutambua mchango wa kuzalisha chakula kwenye Bara letu la Afrika kwa sababu moja ya changamoto tulizonazo ni upungufu wa chakula kwenye baadhi ya maeneo,” amesema.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba