November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia kuzindua matokeo ya Sensa na muongozo wa matumizi ya matokeo hayo

Na Zena Mohamed, Timesmajiraonline, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi Uzinduzi wa Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi, Sensa ya Majengo na Sensa ya Anwani za Makazi  ya Mwaka 2022 pamoja na muongozo wa matumizi ya matokeo hayo.

Uzinduzi huo utakaofanyika katika uwanja wa Michezo wa Jamhuri hapa jijini Dodoma
ambao takwimu zake ndio zitatumika katika kupanga matumizi mbalimbali nchini,wakiwemo wabunge ambao watautumia muongozo huo kujua changamoto za majimbo na kuzitatua.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Oktoba 28,2022 na Waziri wa nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu George Simbachawene wakati akizungumza na Waandishi wa habari huku akiwataka wananchi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi kushuhudia tukio hilo 31 Oktoba, 2022.

“Oktoba 31 ni siku maalum kwa taifa letu hivyo basi hatuna budi kuhakikisha kwa tuliopo Dodoma na mikoa ya jirani tunajitokeza kwa wingi uwanja wa Jamhuri na wale tutakaokuwa mbali tufuatilie uzinduzi huo kupitia vyombo vya habari ili tushiriki pamoja na Mheshimiwa Rais kujua tupo wangapi wakati atakapotangaza Matokeo hayo ya Mwanzo,”amesema

Amesema kuwa uzinduzi huo ni tukio muhimu katika historia ya maendeleo ya nchi ndio maana Serikali imeamua kuhakikisha kunakuwa na uwakilishi wa wananchi wa makundi yote ili waweze kushiriki katika tukio hili la kihistoria.

“Sensa ya Watu na Makazi hufanyika mara moja kila baada ya miaka kumi na matokeo yake ndio yanayotumika katika kufanya maamuzi yote muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi kwa kipindi cha miaka kumi hadi Sensa nyingine,hivyo
Sherehe hizi za uzinduzi wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 zitahudhuriwa na viongozi wote wakuu wa Serikali pamoja na Marais Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Marais wastaafu wa Zanzibar,”amesema

Ameongeza kuwa katika uzinduzi huo pia  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Marais hao wastaafu watatunukiwa tuzo maalum kwa kufanikisha Sensa katika vipindi vya uongozi.

Simbachawene amewataja Waalikwa wengine kuwa ni viongozi wa Serikali wakiwemo mawaziri na manaibu waziri, Makatibu wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Serikali zetu zote mbili, Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Zanzibar, viongozi wa vyama vya Siasa na wawakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii.

“Wageni wengine mashuhuri ni pamoja na Waheshimiwa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao humu nchini, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yakiwemo ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika na Wadau wengine wa Maendeleo,”amefafanua Waziri huyo. 

“Matokeo haya ni muhimu sana kwa makundi yote katika jamii, wafanyabiashara, wakulima, wafugaji na hasa kwa Serikali yetu inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwani Serikali itaweza kupanga mipango yake kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kulingana na idadi, mahitaji na mazingira wanamoishi,”amesisitiza na kuongeza;

Kwetu sisi wananchi wa Dodoma, hii itakuwa historia kwa kuwa itakuwa mara ya kwanza kushuhudia tukio la uzinduzi wa Matokeo ya Sensa ambao ni fursa moja muhimu kwenu kujitokeza kwa wingi kuja kushuhudia uzinduzi huo ambao utapambwa na kila aina ya shamrashamra kuonesha kuwa sio tu kuwa ni tukio la kihistoiria kufanyika Dodoma pia ni tukio linalitokea mara moja tu kila baada ya miaka kumi,”amesema.