December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia: Kunyamaza kwangu kimya si ujinga

*Awaonya wanaoratibu, kushiriki na watakaotekeleza mipango miovu, awashukia
Makulukutabu asema sheria zao zipo, asisitiza wameapa kulinda amani ya nchi

Na Mwandishi Wetu,timesmajiraonline

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa onyo kali wa watu wanaoratibu, kushiriki na watakaotekeleza mipango miovu ya kuvuruga amani ya nchi, huku akiwatahadharisha kwamba kunyamaza kwake kimya sio ujinga, bali ni mtu anayetafakari mambo.

Rais Samia alitoa akizungumza maofisa wa Jeshi la Polisi nchini kwenye kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 tangu kuanzishwa kwa jeshi hilo.

Alisema aliwahi kusema na anarudia tena kwa msisitiko kwamba ukimya wake sio ujinga, na wala kuzungumza sana kwa wale wanaozungumza sana sio uelevu, kuzungumza sana ni udebe tupu tu.

“Na anayenyamaza kimya sio mjinga ni mtu anayetafakari mambo, kwa hiyo kunyamaza kwangu sio ujinga na kuropoka kwao sio uelevu mliponikabidhi dhamana hii niliapa kulinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dhamana yangu pamoja na vyombo vya ulinzi ni kulinda amani ya nchi yetu, hivyo sitakuwa na muhali kwa yeyote anayetaka kuvuruga amani ya nchi yetu,” alionya Rais Samia na kuongeza;

Tumivumiliana kwenye mengi, lakini kwenye kulinda tunu na utulivu wa nchi, nirudie tena sitakuwa na muhali kwa yeyote atakayenikaribisha katika mambo hayo , anayeratibu, anayeshiriki na anayetekeleza mipango hiyo miovu.”

“Nataka niwaambia vikao vyote vya kupanga uovu, uovu utakaopangwa tutaupata , mnapanga sijui kushusha moto mpaka Samia aseme basi, nimekubali ninaondoka . Hiyo Serikali au Serikali ya samaki!

Hiyo ni Serikali ya samaki ndugu zangu, maana samaki kadiri anavyozidi kuwa mkubwa na akili zinakuwaje ndugu zangu? Lakini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haiondoki hivyo,” alisitiza Rais Samia.

Alisema kwa kutumia kofia ya Amiri Jeshi Mkuu wameapa kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba watafanya kila linalowezeka kuimarisha ulinzi na maisha ya Watanzania kwa kuwa wanajua ni jukumu lao.

“Kwa hiyo kwenye wajibu huu wala hatuhitaji kuelekezwa na mtu yeyote nini cha kufanya kwa sababu Katiba yetu ina maelekezo yote ya namna ya kuendesha Serikali yetu na hakuna mtu anayeumia kama wanavyoumia Watanzania haya yanapotokea,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Hatukubaliana na yanayotokea , tunaumia sana kuona haya yanatokea kifo chochote kile kinatuuma Watanzania, hii ni damu yetu Watanzania wengine wanapotaka kuonesha huruma yao, basi tunawasihi wafanye hivyo kwa kufuata makubaliano na mahusiano ya kidoplomasia ya kimataifa kama ilivyoelezwa kwenye Mkataba wa Viena wa Mahusiano ya Kidiplomasia wa mwaka 1961.”

Alisema hilo tamko lililotoka na kuambiwa wafanya moja, mbili tatu, Watanzania wanajua la kufanya na ni imani yake kwamba tamko hilo lililotolewa ni maelekezo. “Hatupo hapa kuelekezwa nini cha kufanya ndani ya nchi yetu.

Tuna katiba, tuna sheria zetu, tuna miongozo tuna mila na desturi zetu, zote zinatuongoza nini cha kufanya ndani ya nchi yetu mambo yanayotokea yanatokea kila nchi. Hayatokei Tanzania , yangekuwa yanatokea Tanzania peke yake yangekuwa yakushangaza.

Lakini yanatokea kila nchi, huku utasikia mtoto kabeba bunduki kaenda kushoot shule watu kadhaa wamekufa, huku nani sijui kachukua nini kaenda kashoot (kupiga), kufa kupo tu, kwa njia yoyote na yanapotokea sisi hatujawahi kuwaambia wewe balozi wetu, ebu waambie hao wafanye…hatujawahi tunatumia mkataba ya kidiplomasia ya kimataifa kama tulivyoambiwa kufanya.”

Rais Samia alisema wengine wasiwe mafundi wakutuelekeza ya kufanya ndani ya nchi yetu, Serikali inaongozwa na falsafa ya maridhiano, kustahimilia, kubadilika na kujenga taifa letu.

“Faisafa hii ilikuja baada ya kuona taifa letu limegawanyika kulikosababishwa na tofauti zetu za kisiasa na kiitikadi, falsafa hii ilikuwa ili watu tutangulize utaifa na Utanzania kwanza kabla ya mengine yoyote kama nchi na Taifa, tumefarijika kuona falsafa hii kwa kiasi kikubwa imeweza kuliunganisha taifa letu.

Hata hivyo, tunapotekeleza falsafa ya R4 sio kuwa tumetupilia mbali sheria za nchi yetu au tumeruhusu utovu wa nidhamu utokee ndani ya nchi yetu. Sheria zipo pale mila na desturi zetu zipo pale pale, miongozo ya kufanya mikutano na mengine yote yapo pale pale, kwa hiyo R4 ni falsafa iliyokuja kuunganisha Taifa na siyo inayoruhusu utovu wa nidhamu kwa baadhi ya watu,” alisema Rais Samia.

Alisema baada ya kazi nzuri iliyofanywa na falsafa hiyo ya kuunganisha Taifa hawataruhusu wala kuvumilia vitendo vyovyote vya kuleta machafuko na mifarakano. Alisema wale wanaojiandaa na machafuko wasisahau mapito waliyopita.

“Ni falsafa hii hii iliyowapa ruksa ya kurudi nchini na tukafumbia mengine yote, njoo tukajenge nchi yetu sasa kama wameishaota mikia, sheria zile zile bado zipo, kule kwetu kuna watu wanaitwa Makulukutabu ni watu wenye hulka za kuishi kwenye tabu tu, kwenye utulivu, kwenye raha kwao sio pahala kwao,” alisema Rais Samia na kuongeza;

“Sasa hapa Tanzania baadhi tunao Makulukutabu, kukiwa na raha nchi imetulia yeye hajaona raha bado , sasa sheria za Makulukutabu pia zipo tutashughulika nao R4 sio sababu ya utovu wa nidhamu, sio sababu ya kukiuka sheria za nchi zipo pale pale, kwa hiyo wasisahau mapito waliyopita.

Alisema Serikali imejitaidi sana kurejesha uhuru wa vyama vya siasa, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa raia kwa ujumla, wale waliokuwa uhamishoni walirejea, waliokuwa na kesi za jina zilifumbiwa macho na waliokuwa jela tuliwatoa sasa wapo uhuru, wanaendelea na shughuli zao zikiwemo za kisiasa, lengo leo likiwa kuwaleta watu pamoja ili kujenga nchi.

“Sasa wale watu wanaposahau yote hayo wanapofanya vitendo vya kutaka kuturudisha nyuma sisi hatutakuwa tayari kuwaruhusu kufanya hivyo, amani na utulivu wa nchi yetu tutailinda kwa gharama yoyote kama nchi zingine zinavyolinda nchi zao na sisi Watanzania tutalinda nchi yetu kwa gharama yoyote ile.”