Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt.Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Fedha, Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na TAMISEMI kuwezesha na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera na mitaala mipya ili ilete matokeo yaliyokusudiwa.
Dkt.Samia amesema hayo jijini hapa leo Februari Mosi, 2025 wakati akizindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 – Toleo la 2023.
Amesema kuwa uwepo wa Sera ya Elimu na Mitaala Mipya pekee haviwezi kuleta matokeo ya elimu yanayotakiwa bali kitakachosaidia kuleta matokeo ni utekelezaji wake.
Ameeleza kuwa katika maboresho yatakayofanywa, Walimu lazima wazingatiwe ambapo serikali itaendelea kuajiri Walimu wenye sifa na kuwapa mafunzo stakihi ili waweze kuendana na mwelekeo wa sera hiyo aidha serikali itapitia upya maslahi ya kada ya Ualimu nchini.
“Dhamira ya mabadiliko ya Sera ya Elimu na Mafunzo ni kumuandaa kijana anayejiamini na mwenye nyenzo stahiki za kukabiliana na ushindani wa kikanda na kimataifa ili aweze kutumia na kunufaika na utajiri wa rasilimali zilizopo nchini.
“Kwa muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kuongeza Pato la Taifa hadi kufikia Dola bilioni 700, ni wazi kwamba Sera hii itakuwa nyenzo muhimu kwa kuongeza wigo wa watenda kazi wenye ujuzi watakaoshiriki kujenga uchumi wa nchi,” amesema Rais Samia.
Ameeleza kuwa, Sera na mitaala imewekewa msisitizo wa elimu ujuzi na ufundishwaji wa somo la ujasiriamali ambalo litamuwezesha kijana kupata misingi ya biashara na kutoa mchango kwa taifa, pia Sera ina lengo la kutambua na kurasimisha ujuzi na stadi zinazopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo uliopo.
Vile vile, Ili kumuandaa kijana kushindana kikanda na kimataifa, Sera hiyo pia itawasaidia wanafunzi kupata elimu ya lugha mbalimbali za kimataifa mbali na kiingereza ikiwemo; kichina, kifaransa na kiarabu kwani ndizo lugha zinazoendesha uchumi duniani.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Philip Mpango amesema kuwa Sera ya Elimu ni kanuni ambazo zinaongoza nchi kuweza kufikia maamuzi kuhusu maendeleo ya elimu na kufikia malengo ya nchi pia, ndiyo mwongozo wa kuandaa mtaala wa elimu unaotumika kufundishia wanafunzi.
“Sera hii mpya itatuwezesha kubadili mfumo wetu wa elimu ili kuweza kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi wa kumudu mabadiliko ya teknolojia”,amesema Dkt. Mpango.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu na Mafunzo, Profesa.Adolf Mkenda amesema kuwa chimbuko hilo kubwa la kihistoria la kuwa na sera mpya ya elimu na mitaala iliyoboreshwa limetoka kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Ambapo amesema sera hiyo ilizinduliwa mwaka 2015, mwaka wa uchaguzi chini ya Katibu Mkuu, Profesa. Sifuni Mchome.
Amesema wakati wa kukusanya maoni waliangalia ama waende na miaka saba ya elimu ya msingi na miaka saba ya elimu ya lazima au waende na miaka sita ya elimu ya msingi na miaka 10 ya elimu ya lazima ambayo imeshapitishwa, wakaona miaka 10 ni sahihi zaidi ukilinganisha na nchi jirani ya kesho ambayo ni miaka tisa ya msingi na miaka 12 ya lazima ambapo pia waliangalia nchi nyingine.
More Stories
Serikali yaboresha sekta ya elimu Ulyankulu
Sababu za matukio ya ukatili zatajwa
Upungufu wa maji Mji Korogwe, HTM waeleza mikakati yao