January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia azindua kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amezindua rasmi kampeni  ya Maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 huku akiziagiza taasisi na sekta mbalimbali kusimamia vyema fedha zitakazotumika katika mapambano dhidi ya UVIKO 19 ambazo zimeelekezwa kwenye miradi mbalimbali ya kuindoa jamii ya watanzania kwenye janga la maambukizi ya UVIIKO 19.Rais Samia pia amewataka watakaopewa  Fedha hizo wakazitumie kwa malengo yaliyokusudiwa huku akiwaonya wale wenye mpango wa kujaribu kutumia fedha hizo kwa maslahi yao binafsi waache mara moja.

“Wale waliopanga kudokoa fedha ninawaonya,na wanaotaka kunijua rangi zangu wajaribu kudokoa fedha hizi .”amesisitiza Rais Samia

Rais Samia ametoa kauli hiyo hii leo Jijini Dodoma wakati akizindua kampeni hiyo  iliyohudhuriwa na  viongozi mbalimbali wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Visiwani Zanzibar huku vikiwemo  Vyama 13 vya Siasa,Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Serikali ,Viongozi wa dini pamoja na  Mashirika ya Kimataifa ,Shirika la Fedha Duniani ( IMF) na Shirika la Afya Duniani (WHO) .

Katika mapambano dhidi ya UVIKO 19 ,Serikali imepokea mkopo nafuu wa dola milioni 579 sawa na sh. trilioni 1.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya mpango huo kwa kipindi cha miezi tisa Fedha ambazo zimetolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

“ Wenzetu  waliopokea fedha kama hizo zote walielekeza katika ununuaji wa Chanjo na vifaa vya kujikinga na korona ila kwa upande wa Tanzania inaelekezwa kwenye miradi ya kukabiliana na janga la UVIKO 19 …,maana ili tuweze kukabiliana na janga hili la korona lazima  kuwe na maji,kupunguza masafa ya wanafunzi kubanana  ,kuwepo kwa vituo vya afya vingi vitakavyoweza kutoa huduma ipasavyo kuanzia ngazi ya tarafa ili corona ikija vituo vinakuwa vipo kuanzia ngazi ya  chini hadi  juu.”amesema Rais Samia

Aidha ametoa wito kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa hiyo na  kuzalisha bidhaa ambazo zitatumika kwenye utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo simenti,mabati kwani kuna madarasa 15,000,vituo vya afya 200 vinaenda kujengwa na kufanyiwa ukarabati hivyo vinahitaji mabati mengi na saruji.

.”Rai yangu kwa watekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa mashule ,vituo vya afya Na miradi ya maji kuwatumia  wakandarasi wenyeji waliopo hapa nchini kwani wakandarasi wetu walikuwa wanalia miaka mingi kukosa kazi za serikali ,

“Sasa wakandarasi kazi hizi hapa tunaomba sana na wao wawe wakandarasi bora,wenye sifa,ambao watafanya kazi kwa umakini na ufanisi na uwajibikaji Mkubwa..,sasa ni wakati wa wakandarasi wa ndani kwa sababu fedha hii ilipwe kwao na iweze kuzunguka  kwenye uchumi wa ndani hapa nchini.”

Pia ametoa rai  kwa wasimamizi hao huku akiwataka kutumia na kukamilisha miradi kwa muda uliopangwa huku akisema asingependa washindwe kutumia fedha hizo kwa visingizio mbalimbali huku akiagiza ,utaratibu wa kupata msamaha wa kodi uondolewe kwa vifaa vya bidhaa zitakazoagizwa kutoka nje ya nchi yetu katika mpango huo.

Vile vile amemuagiza  Waziri wa Fedha na Mipango na kuagiza kusimamia katika suala hili kuwa mwepesi kutoa msamaha ya kodi  kwa yale yatakayoagiza nje  anayekuja kwenye miradi hii.Rais Samia vile vile amemuagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za  serikali pamoja na Mkaguzi wa ndani wa hesabu za ndani kufuatilia kwa umakini matumizi ya fedha hizi kwa malengo yaliyokusudiwa na kwa thamani halisi.

Alisema pia Kamati za Bunge zinapaswa kuhakikisha kusimamia matumizi hayo huku akisema ,katika kutembelea miradi muende mkasimamie matumizi ya fedha hizo.

“Vile vile naagiza kusiwe na utitiri wa kamati za kusimamia badala yake ziwe ni Kamati ziwe kamati za wataalamu iwe kamati ya Mikoa itakayosimamiwa hadi wilayani itakayosimamia miradi hii.”alisisitiza

Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt.Philip Mpango alisema UVIKO 19 umeleta hasara nchini kwani umepoteza watu wengi wakiwemo wataalam mbalimbali huku familia nyingi zikiteketea na nyingine kupoteza waliowategemea.

“Kama tunavyofahamu UVIKO 19 umepoteza watu wengi na familia nyingine zimepoteza mkimu familia na nyingine nyingi zilikuwa naangalia takwimu zikanitisha kidogo ,inakadiriwa karibu watu milioni moja wameingia kwenye lindi la umasikini kwa ghafla kwa sababu ya UVIKO 19,

“Tumepoteza wataalam wa afya na wataalam wengi hii ni hasara kubwa kwa Taifa ,lakini mahitaji ya dawa ,vifaa tiba kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa yamekuwa ni makubwa sana ,lakini pia biashara ya utalii imeanguka baada ya nchi nyingi kuweka zuio la kusafiri kwa ajili ya kujikinga ,pia tumekuwa na hofu na mashaka ya kuambukizwa UVIKO 19 katika maeneo mbalimbali”alisema

Dkt.Mpango amemshukuru Rais Samia kwa kupambana na UVIKO 19kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Asante  sana mama kwa ujasiri wako wa kutafuta chanjo na kuongoza zoezi la kuchanja,umetimiza wajibu wako kama kiongozi mkuu wa nchi yetu wa kulinda uhai wa wananchi wako ,tunakushukuru sana..,umetafuta fedha ili nchi yetu isizidi kudorora “

Pia Dkt.Mpango amemshukuru  Waziri wa Fedha Dkt.Mwigulu Nchemba kwa kufanya kazi ya kuhakikisha maagizo ya Rais Samia yanatekelezwa na kusimamia vyema  kwa majadiliano na Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Mwinyi alisema Mpango huo ni katika juhudi za Rais Samia  kuendeleza misingi ya utawala bora hapa nchini kwa kuwa na  misingi ya kuwapatia wananchi taarifa za nchi yao.

“Baada ya kupata fedha hizi ungeweza kukaaa ofisini na kupanga mipango yako,lakini ukaona haitoshi nakuamua kuleta taarifa ya matumizi ya fedha hizi kwa wananchi.”alisema Dkt.Mwinyi

Dkt.Mwinyi amemshukuru Rais Samia kwa kuiwezesha Zanzibar  kupata mgao wa fedha hizo huku akiahidi fedha hizo kutumika kwa malengo yaliyowekwa nakwamba atahakikisha kunakuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha hizo.

Awali Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.Mwigulu Nchemba alisema nia ya Rais Samia ni kutafuta suluhisho la muda mrefu la kukabiliana na UVIKO 19 kwa maslahi mapana ya wananchi wake na Taifa kwa ujumla.

Alisema kwa kutumia fedha hizo Serikali inakwenda kujenga miundombinu mbalimbali katika sekta za maji,elimu,Utalii na afya ambayo itakapokamilika inakwenda kuokoa maisha ya wananchi dhidi ya UVIKO 19.

XXXXX