January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia azindua Chuo Cha VETA Igunga

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

RAISI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameanza ziara ya siku 2 Mkoani Tabora kwa kuzindua Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA) wilayani Igunga Mkoani hapa.

Akizungumza na umati wa wakazi wa Wilaya hiyo na Mkoa mzima wa Tabora amepongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa usimamizi mzuri wa vyuo hivyo.

Amesema dhamira ya serikali yake ya awamu ya 6 ni kuhakikisha vyuo vya aina hiyo vinajengwa katika Wilaya zote nchini na katika kila Mkoa.

Amebainisha kuwa vyuo hivyo ni muhimu sana kwa vitasaidia kuwapa vijana ujuzi wa aina mbalimbali utakaowawezesha kujiajiri.

‘Serikali imedhamiria kukuza ujuzi wa vijana na kuongeza wataalamu watakaosaidia kuchochea miradi ya kimkakati ikiwemo kufanikisha programu ya Jenga Kesho iliyo Bora, amesema.

Rais Samia amepongeza Wizara hiyo kwa kujenga vyuo 64 hadi sasa na kuwataka kuendelea kusimamia vizuri miradi hiyo katika Wilaya na Mikoa yote.

Aidha Rais Samia amepongeza Viongozi wa Mkoa huo kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo hali ambayo imepelekea kupungua malakamiko ya wananchi.

Amewataka wakazi wa Mkoa huo kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kupata maendeleo makubwa.

Amesisitiza kuwa serikali imeendelea kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima ili walime maeneo makubwa zaidi na kujipatia kipato.

Ameongeza kuwa jukumu la serikali ni kuendelea kutafuta masoko zaidi ili mazao yote ya wakulima yapate soko na yale yatajayokosa soko serikali itayanunua.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ameeleza kuwa Chuo cha VETA Igunga kimegharimu kiasi cha sh bil 2.6 na ni Chuo cha 5 kujengwa katika Mkoa huo.

Amebainisha kuwa serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa vyuo hivyo ili kuwezesha vijana wengi kupata ujuzi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa VETA Anthon Mzee Kasola ameeleza kuwa hadi sasa vyuo 33 vimeshajengwa na kukamilika na vyuo 64 ujenzi unaendelea katika Wilaya mbalimbali.

Amefafanua kuwa kukamilika kwa Chuo cha Igunga kutawezesha vijana zaidi ya 120,000 kupata fursa ya kujiunga na Chuo hicho.