May 4, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atoa pole kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa Watanzania wote waliofikwa na athari ya mafuriko katika maeneo kadhaa kama vile Rufiji, Morogoro na mkoani Arusha, akisema serikali yake imeendelea kuchukua hatua kadhaa kukabiliana na hali hizo ikiwa ni pamoja na kupeleka misaada ya chakula na dawa.

Rais Samia pia ametoa pole kufuatia ajali ya gari ya wanafunzi iliyotokea jijini Arusha na kusababisha vifo vya wanafunzi kadhaa kutokana na uzembe wa dereva wa basi hilo. Dk. Samia alisema serikali itafanya uchunguzi wa kina kubaini sababu ya mafuriko hayo.

“Baada ya mvua hizi na hali ya kawaida kurejea, serikali itafanya uchunguzi wa kina kubaini sababu halisi za mafuriko kwenye maeneo hayo ili tuweze kuchukua hatua zitakazoondoa tatizo hili kwa muda mrefu. Niwaombe wananchi kuwa watulivu na kushirikiana na watendaji wa serikali kwenye maeneo yao. Pia niwaase wananchi kuendelea kuchukua tahadhari pindi wanapofika sehemu zenye maji yanayotembea iwe wanapita kwa miguu au kwenye magari ili kuepusha athari zozote zinazoweza kusababisha vifo kwa wananchi wetu,” Alisema Dk. Samia.

Aidha Dk. Samia aliwataka Watanzania kuendeleza utamaduni kutoa misaada kwa wahitaji, sambamba na viongozi wa serikali kutumia nafasi zao kwenye majukwaa kuunganisha wananchi na kulisemea ili wananchi wawaelewe na kupata faraja.