Na Lubango Mleka, TimesMajiraOnline Igunga.
WANANCHI wa Kata ya Mwisi Wilayani Igunga Mkoani Tabora, wameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia shule ya sekondari ya Mwisi kiasi milioni 642 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 8, mabweni 3 na matundu 12 ya vyoo.
Baadhi ya wananchi hao waliotoa pongezi hizo akiwemo Asha Hamis amesema kuwa fedha hizo kwa Kata ya Mwisi za ujenzi wa madarasa zimetatua changamoto ya wazazi na wananchi kuchangishwa fedha za ujenzi mara kwa mara.
Hivyo fedha zinazotolea na Rais zitatatua changamoto katika sekta ya elimu,afya na maji jambo ambalo limewapa matumaini na kuendelea kuiamini serikali ya awamu ya sita.
“Natanguliza shukrani zangu za dhati kwa mama yetu Samia kwa jitihada anazozifanya kwa Kata yetu ametoa kama milioni 642 na sasa hivi kazi inaendelea pale shuleni ya kujenga madarasa, mabweni na matundu ya vyoo yaani kazi inafanyika nzuri sana kiasi kwamba hata ukifika wakandarasi na wanafanya kazi muda wote pia diwani Jambeck na walimu wanasimamia kazi muda wote,” amesema Kalwisha kada wa CHADEMA.
Huku George Maige amesema kuwa yeye ni Mwanachadema, katika miradi ya maendeleo ni lazima waseme ukweli akianza kwa siku za nyuma suala la elimu wanachangishwa fedha kila kaya lakini majengo yalikuwa hayaendi.
“Katika utawala wa Rais Samia madarasa, mabweni yanaota kama uyoga, leo nimetembelea hapa shuleni nimeona kazi zinapigwa, kwa kweli inatia moyo sana, ili kuwa na maendeleo bora inaitaji kuwa na viongozi bora, Diwani Jambeck anajitoa sana kufuatilia miradi yote hapa katani,”.
Naye Kwandu Tungu, amewataka wananchi wenzake,wanafunzi na walimu kusimamia miradi hiyo na kuitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu, na kuhakikisha kuwa atakaye ihujumu basi anakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Kwa upande wake Diwani wa kayta hiyo Ahamed Ibrahim Jambeck, amempongeza Rais Samia kwa kuwaamini watendaji wake katika ngazi ya chini na kuendelea kuwapatia fedha nyingi za miradi ikiwemo miradi ya afya, elimu, maji na umeme.
” Kwanza kabisa nitoe shukrani zangu kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini viongozi wake katika ngazi za chini kwa usimamizi wa miradi, fedha hizi tulizopewa zinafanya kazi ya ujenzi wa madarasa nane, mabweni matatu na matundu 12 ya vyoo na mnajione wenyewe waandishi jinsi kazi inavyo kwenda na kwa ubora unaotakiwa, pia tunatarajia majengo haya yote yakamilike kwa wakati uliopangwa,” amesema Jambeck.
Amesema kuwa, mradi huo unatoa ajira za muda kwa zaidi ya wananchi 300 ambao ni mafundi, vibarua na wapishi, huku baadhi ya wafanyabishara pia wananufaika na mradi huo kwa kuuza bidhaa kwa wafanyakazi na vifaa vya ujenzi kwa mradi.
” Pia naishukuru Serikali kwani ilitupatia milioni 100, ambazo tumejenga bwalo kubwa la kisasa ambalo litatumiwa na wanafunzi, nitoe rai kwa walimu, wazazi na wananchi kwa ujumla waendelee kuiamini serikali yao pamoja na sisi viongozi wao kwani tukishirikiana kwa pamoja kuisimamia miradi hii itakuwa bora zaidi na kudumu kwa muda mrefu,” amesema Jambeck.
More Stories
Nani kuwa mrithi wa Kinana CCM?
Watendaji Songwe wapatiwa mafunzo uboreshaji daftari la mpiga kura
Samia: Mwaka 2024 ulikuwa wa mafanikio