December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania

*Amwaga pesa knockout ya Mama Magomeni

*Wadau wa ngumi washushukuru sapoti ya Rais Samia

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametia mkono katika maendeleo ya mchezo wa masumbwi nchini Tanzania kwa kuamua kutoa zawadi kwa Watanzania wote walioshinda katika mapambano ya ngumi yanayofahamika kama ‘Knockout ya Mama’, yaliyofanyika katika Ukumbi wa City Centre Hall Magomeni, Usalama, jijini Dar es Salaam.

Katika mapambano hayo, mabondia wa Tanzania wasiopungua nane walifanikiwa kupanda ulingoni kucheza na wapinzani wao kutoka nchi mbalimbali kama vile Philippines, Ghana na Afrika Kusini, Uganda na Angola.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Uzalishaji na matangazo wa Mafia Boxing Promotion, Omary Clayton, alisema Rais Samia ameingiza mguu kwenye mchezo wa masumbwi wakati huu ambao wadau na mabondia wana kiu ya kufanya makubwa na kuitangaza nchi katika nyanja za Kimataifa.

Alisema Rais Samia aliamua kutoa zawadi nono kwa mabondia wa Watanzania watakaopata mikanda pamoja na wale watakaoibuka washindi katika mapambano ya kawaida.

“Mama amekuja kwenye masumbwi kwa nguvu zote, ambapo kila Mtanzania alishinda katika pambano lake ameshikwa mkono tukiamini huu ni mwendo mzuri katika juhudi za kuuinua mchezo wa ngumi nchini kwetu”

“Kwa ujumla yamefanyika mapambano 11, ambayo nane ni ya Kimataifa, huku matatu yaliyosalia ndio yameshirikisha watanzania watupu ambapo pia zawadi ya Knockout ya Mama ilihusika,”Alisema Omary.

Baadhi ya mabondia wa Tanzania waliopata zawadi ya Rais Samia ni pamoja na Issa Nampepeche aliyemchapa kwa Knockout mpinzani wake Joseph Masunga na kujinyakulia Sh Milioni 3, Mchanja Yohana amepata Sh Milioni 1.5 kwa kumpiga kwa pointi mpinzani wake Michael Aban wa Ghana. Wengine ni Mtanzania Salmin Kassim aliyeibuka na Sh Milioni 3 kwa kumpiga kwa Knockout mpinzani wake Non James wa Ufilipino, huku Mtanzania mwingine Ibrahim Mafia yeye akizoa Sh Milioni 7 baada ya kushinda mkanda wa WBC Africa Belt dhidi ya bondia kutoka Ghana, Enoch Tetty katika pambano la raundi 9.

Naye Mtanzania Kalolo Amiri amepata sh milioni 1.5 za Rais Samia kwa kushinda kwa pointi dhidi ya mpinzani wake Bono Koane wa Afrika Kusini, huku Mtanzania mwingine Said Mohamed maarufu kama Chino akiibuka na mkanda wa IBA Intercontinental Championship kwa kumchapa kwa pointi mpinzani wake Kusanda Komanisa wa Afrika Kusini na kuondoka na Sh Milioni 5 ya Knockout ya Mama.

Mwishoooooooooooooooo