December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ateta na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu UN

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira,Online Nairobi

RAIS Samia Suluhu Hassan, amekutana na kufanya mazungumzo na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Balozi Xia Huang Jijini Nairobi.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Huang amewasilisha salamu za pole za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres kwa Rais Samia kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Magufuli na pongezi kwa Rais Samia kupokea kijiti cha Urais akiwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais nchini Tanzania.

Balozi Huang amesema Umoja wa Mataifa wanayo matumaini makubwa na uongozi wa Rais Samia katika kuiongoza Tanzania na kuendeleza ajenda za ukanda wa Maziwa Makuu ambazo ni kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi na pia kuendeleza juhudi za kulinda amani na kuimarisha usalama.

Ameipongeza Tanzania kwa mchango na ushirikiano mkubwa inaoutoa kwa Umoja wa Mataifa katika juhudi za kulinda amani na kuimarisha usalama katika maeneo yote yenye mapigano na makundi yanayohasimiana na ameahidi kuwa umoja huo utaendelea kushirikiana na Tanzania kulinda amani ili maendeleo ya jamii na uchumi yastawi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Kwa upande wake, Rais Samia amepokea salamu za pole na pongezi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , Guterres na amemhakikishia kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na umoja huo katika juhudi za kulinda amani na usalama katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Rais Samia amesema hali ya ulinzi na usalama na demokrasia nchini Tanzania ni nzuri na ameomba Umoja wa Mataifa kuendeleza jitihada za kulinda amani na usalama katika maeneo yote yenye matatizo.

Aidha, Rais Samia alitoa wito kwa umoja huo kuushawishi Umoja wa Ulaya (EU) kuondoa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Burundi.