Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
RAIS Samia Suluhu Hassani amempongeza mfanyabiashara, Alhaji Aliko Dangote ambaye amewekeza katika kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa saruji Mkoani Mtwara na amemhakikishia kuwa Serikali itahakikisha uwekezaji wake na wawekezaji wengine unalindwa kwa manufaa ya pande zote mbili.
Rais Samia ametoa kauli hiyo Ikulu, jijini Dar es Salaam alipokuta na kufanya mazungumzo na mfanyabiashara Alhaji Dangote.
Amempongeza kwa uwekezaji alioufanya hapa nchini na kumuagiza Waziri wa Uwekezaji, Geoffrey Mwambe, Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof. Kitila Mkumbo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Masauni ambao walihudhuria mazungumzo hayo kufanyia kazi changamoto zote zinazokikabili kiwanda cha Dangote ili kiendelee kuzalisha inavyotakikana na kuleta manufaa yaliyokusudiwa.
Baada ya mazungumzo hayo, Alhaji Dangote alimpongeza Rais Samia kwa kuchukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara nchini Tanzania na alimuahidi kuwa kampuni yake ambayo imewekeza hapa nchini kiasi cha Dola za Marekani Milioni 770 (sawa na shilingi Trilioni 1.761) itaendelea kuwekeza katika maeneo mengine ikiwemo mpango wake wa kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea.
“Tutaendelea kuwekeza Tanzania ili kuzalisha ajira, mapato ya nchi na kuinua ustawi wa wananchi wa Tanzania, nadhani anahitaji kuungwa mkono katika hili na tumemuahidi kuwa tutaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa hapa Tanzania ili kuunga mkono anachokifanya, sisi tutazalisha ajira,”amesema Alhaji Dangote.
Amesema, kutokana na kubadilika na kuimarika kwa mazingira ya biashara nchini Tanzania atawahimiza wafanyabiashara na wawekezaji wenzake kuwekeza Tanzania kwa kuwa Serikali ipo tayari kushirikiana nao.
More Stories
ACT-Wazalendo,waitaka Polisi kutobeba chama kimoja
Gavu aanika miradi iliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita Geita
RC Makongoro: Samia aungwe mkono nishati safi ya kupikia