January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia ataka Wizara ya Nishati kuongeza kasi usimamizi wa miradi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Moro

RAIS Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Nishati kuongeza nguvu katika kusimamia miradi yote ya nishati ili ikamilike kwa wakati na hivyo kuwawezesha wananchi kupata nishati ya uhakika.

Rais Samia alitoa agizo hilo juzi, Agosti 06, 2024 wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

“Nimejionea mwenyewe wakati naenda Kilosa tofauti iliyokuwa ikionekana maeneo ambayo hayana umeme na yale yenye umeme ambayo yameshamiri kwa shughuli za biashara, hii inaonesha umuhimu wa nishati katika maeneo yote nchini.” Alisisitiza Dkt.Samia

Aidha, Rais Samia aliutaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukamilisha mapema kupeleka umeme kwenye Vijiji vilivyobaki na kuongeza kasi ya kusambaza umeme kwenye Vitongoji ili wananchi waweze kufanya kazi za maendeleo.

Aidha, alisisitiza kuwa uwepo wa umeme wa uhakika kutoka Bwawa la Julius Nyerere kunaufanya Mkoa wa Morogoro kuwa sehemu sahihi ya uwekezaji.

“Morogoro sasa ina umeme wa uhakika, hali inayovuta uwekezaji ndani ya Mkoa.” Aliongeza Rais

Akizungumzia kuhusu miradi ya umeme vijijini Mkoa wa Morogoro, Dkt. Samia amesema kupitia Wakala wa Nishati Vijijini Serikali imepeleka umeme kwenye Vijiji 621 kati ya Vijiji 669.