Na Penina Malundo, timesmajira,Online
RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa pendekezo la kuundwa kwa kikosi kazi cha kitaifa kitakachoratibu dira na mwenendo wa kitaifa wa kuchakata sera na kuleta matokeo chanya ya kuwa na asilimia 90 ya watanzania watakaokuwa wakitumia Nishati safi ya kupikia katika kipindi cha miaka 10 ijayo.
Rais Samia aliyasema hayo leo, wakati ufungua wa Kongamano la Kitaifa la Nishati Safi ya Kupikia ‘Tanzania Clean Cooking, Conference’ lililofanyika jana, jijini Dar es Salaam.
Amesema sehemu kubwa ya jamii nchini hasa maeneo ya Vijijini imekuwa ikikata miti kwa ajili ya kuni kutokana na bei ya mkaa kuwa chini na hivyo kuhimiza upandaji wa miti ya matunda ambayo wengi wao hawatoweza kuikata bila sababu ya msingi na kwafanya watumie nishati ya gesi kupikia.
Rais Samia Suluhu Hassan aliielekeza wizara ya Nishati inayoongozwa na Waziri January Makamba kuhakikisha ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mapema mwaka 2023, nishati safi inasambazwa kwenye taasisi kubwa.
“Wakati nikiwa Makamu wa Rais, na nina bahati na January kwenye mambo ya mazingira. Kule nilimuelekeza taasisi zinazohudumia zaidi ya watu 300 lazima watumie nishati safi… akiwa kule hakukaa muda mrefu akatoka hatukulitekeleza. Nakuelekeza tena leo, lilelile kwamba taasisi zile; jela, shule, vikosi vya ulinzi zianze sasa kujielekeza kwenye nishati safi ya kupikia.” ameagiza Rais Samia
“Nimemsikia hapa Dada yangu Tibaijuka akisema katika kitabu chake alichokiandika kwamba alisisitiza umuhimu wa kupanda miti ya mkaa, sasa mimi nataka kubadili fikra tupande miti ya matunda maana hiyo huwezi kuikata bila sababu maalum, tuwahimize watu watumie nishati safi ya kupikia,” amesisitiza Rais Samia.
Aidha, ameitaka Wizara ya Nishati kuhakikisha inahamasisha matumizi hayo ya nishati safi ya kupitia kwa taasisi mbalimbali nchini ikiwemo Magereza, Mashule na Maofisini ili kupunguza matumizi ya mkaa ambao unapatikana kutokana na miti ambayo husaidia uhifadhi wa mazingira.
Kuhusu shida ya maji, Rais Samia amesema tayari mkataba wa ufanyaji kazi umesainiwa ili kukamilisha ujenzi wa Bwawa la kidunda litakalosaidia kupunguza kero ya maji jijini Dar es Salaam na maeneo jirani na kusaidia kusongesha mbele gurudumu la maendeleo.
Awali Prof. Anna Tibaijuka amesema Serikali kuweka utaratibu mzuri wa kibiashara kwa wauzaji wa nishati ya gesi ili waweze kuyafikia maeneo mengi hasa ya vijijini.
Amesema sehemu kubwa ya wananchi wa Vijijini wamekuwa wakikumbana na adha ya utafutaji wa kuni kwa ajili ya kupikia kitu ambacho kimekuwa kikiwapotezea muda mwingi wa kufanya shughuli za kuinua vipato vyao na hivyo kushindwa kumudu gharama za maisha.
“Mimi mwenyewe ni muhanga wa watu walikuwa wakikumbana na adha ya utafutaji kuni hivyo naelewa fika suala hili kama kweli mjadala huu unalenga kuleta unafuu ni wazi kwamba tunahitajika kuchukua hatua rafiki kwa kuwashirikisha Wafanyabiashara wa gesi,”amesema Tibaijuka.
Amesema, ipo haja pia ya kuwazua jinsi ya kukishughulikia jambo hilo la nishati safi ya kupikia upande wa gharama kwani matumizi ya mkaa ni rahisi kutokana na wafanya biashara kuweka mazingira rafiki kwa kuuza mafungu kulingana na hali ya Wananchi.
Waziri wa Nishati, January, amesema kongamano hilo linalenga kuwaokoa maelefu ya Watanzania ambao wamekuwa wakiathirika kutokana na kutumia nishati inayotokana na kuni, mkaa na mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama.
Takwimu zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu 30,000 wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na kutumia nishati ya kuni na mkaa ambayo, kiafya sio salama lakini kutokana na changamoto mbalimbali imewalazimu kutumia.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa