Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Mkinga
RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Mkinga mkoani Tanga kutunza mazingira kwenye Safu ya Milima ya Usambara Tao la Mashariki ili kuhakikisha Mto Zigi haukauki, na Mradi wa Maji Mkinga- Horohoro unakuwa endelevu.
Ameyasema hayo leo Februari 27,2025 alipoweka Jiwe la Msingi Mradi wa Maji Mkinga- Horohoro kwenye hafla iliyofanyika Kijiji cha Manza, ambapo mradi huo ni moja ya miradi mikubwa nchini ukigharimu sh.bilioni 35.4.
Dkt.Samia amesema mradi huo unatumia fedha nyingi kuujenga, hivyo hautakuwa na maana kama hautakuwa endelevu kwa wananchi kuharibu vyanzo vya maji Mto Zigi, na akataka wadau washirikiane kuona vyanzo haviharibiwi, hasa watu wanaochimba madini kiholela.

“Ili mradi uweze kuwa endelevu,viongozi mnatakiwa kujipanga kuhakikisha chanzo cha maji hakiharibiwa na kusababisha maji kukauka.Taasisi zishirikiane ili kulinda chanzo hicho ikiwemo kudhibiti uchimbaji madini kwenye vyanzo”amesema Dkt. Samia.
Dkt.Samia amesema ahadi yake nchi nzima ni kusambaza maji safi na salama kwa wanachi. Na kusema anajua muda wa kumaliza Mradi wa Maji Mkinga- Horohoro ni Oktoba, mwaka huu, lakini anatamani wananchi wapate maji, na wasisubiri mradi wote ukamilike, na kuagiza angalau miezi miwili ijayo wananchi wapate maji hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt.Batilda Burian alimshukuru Rais Dkt.Samia kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya mradi huo wa maji na kusema utawasaidia wananchi kuondokana na adha ya shida ya maji.

Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) CPA Amos Makalla amesema tangu akiwa Naibu Waziri wa Maji walikuwa wana mipango ya kuyatoa maji Mto Zigi ili yaende Mkinga, lakini walishindwa, hivyo Rais Dkt. Samia ameweka rekodi ya aina yake.
Mbunge wa Mkinga na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula alisema Mradi wa Maji Mkinga- Horohoro ni mfupa uliowashinda viongozi wengi, na ilikuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi. Mradi huo ni mkombozi kwa wananchi wa Mkinga, na utawasaidia kupata wawekezaji wengi watakaoweka vitega uchumi, kwani Mkinga ndiyo eneo kubwa la wazi kwa sasa katika mkoa wa Tanga kufanya uwekezaji

Kitandula amesema asilimia zaidi ya 90 maji ya Mto Zigi yanatoka kwenye wilaya za Muheza na Mkinga vijiji vya Bosha na Kigongoi, lakini kuna watu wanachimba madini kiholela, hivyo watu hao wadhibitiwe, na lazima maji yalindwe kwa kuzuia watu kuchimba madini.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema kuna wakati Kitandula alitaka kuzuia bajeti ya wizara hiyo isipite kwa ajili ya kutetea Mradi wa Maji Mkinga- Horohoro upatiwe fedha, na alimuahidi atakuja kuangalia, na alipomueleza Rais Dkt. Samia mradi huo unahitaji fedha nyingi, Rais alimjibu, kwenye kuwasaidia wananchi wapate maji, hawawezi kuangalia gharama
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri alisema mradi huo unaojengwa na Mkandarasi mzawa, Allan Makame chini ya kampuni yake ya STC construction company Ltd yenye Makao Makuu, utakaogharimu sh. bilioni 35.4, utawasaidia wananchi 57,332 kwenye vijiji 37, huku mtandao wa mabomba ukiwa kilomita 196, na utakamilika Oktoba 2025.

More Stories
Oryx yaanika jitihada za kuunga mkono kampeni ya nishati safi ya kupikia kwa Rais Samia
Uwekezaji uliofanyika serikali awamu ya sita umezalisha ajira 523,891 nchini
Dkt. Matarajio: Tunataka Nishati ya Petroli iwe injini ya maendeleo