Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline, Dodoma.
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ,ameridhia watumishi walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti takribani 14,516 warejeshewe michango yao tu ambapo inatarajia kulipa zaidi ya Sh.bilioni 46 kwa watumishi hao kuanzia Novemba Mosi Mwaka huu.
Kauli hiyo imetolewa jijini hapa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,ajira vijana na wenye ulemavu Prof.Joyce Ndalichako wakati akitoa Tamko la Serikali kwa Waandishi wa habari kuhusu maamauzi ya kuwarejeshea michango iliyopo kwenye Mifuko ya hifadhi ya Jamii ya PSSSF na NSSSF Watumishi hao.
Ndalichako amesema kuwa watumishi hao walioondolewa kazini mnamo Mwaka 2016 na 2017 baada ya Serikali kufanyika zoezi maalum la uhakiki wa Vyeti kwakushirikiana na Baraza la Mitihani la Taifa NECTA na kubainika wakiwa wamegushi Vyeti.
“Serikali iliendesha zoezi hilo maalum la uhakiki wa vyeti kwa kushirikiana na Baraza la Mtihani la Taifa (NECTA)mnamo Oktoba 2016 hadi Aprili 2017,”amesema.
Ndalichako ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameridhia watumishi wote walioondolewa kazini kwa kughushi vyeti warejeshewe michango yao kwa asilimia tano waliyokatwa kwenye mishahara na kuwasilishwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
Amesema kuwa kufuatia maelekezo hayo mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSSSF na NSSF itarejesha michango ya wafanyakazi iliyowasilishwa kwenye mifuko hiyo bila kuhusisha michango ya mwajiri.
“Mtumishi husika atatakiwa kwenda kwa aliyekuwa mwajiri wake akiwa na picha mbili za passport size, nakala ya taarifa za kibenki,nakala ya kitambulisho cha taifa au mpiga kura au leseni ya udereva”amesema Ndalichako.
Amesema kuwa kufuatia kuondolewa kwenye utumishi wa umma watumishi hao wamekuwa wakitumia njia mbalimbali ikiwa pamoja na kutumia Vyama vya Wafanyakazi kuomba walipwe mafao kutoka kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii.
“Wakati wa maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi duniani Mei 1 mwaka 2022 Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA)kupitia risala yao ,waliwasilisha ombi kwa Rais aangalie namna ya kuwafuta jasho watumishi hao”
“Kufuatia maombi hayo Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake kwenye siku ya Wafanyakazi duniani lielekeza kufanyika kwa uchambuzi ili kuona namna gani ambavyo serikali inaweza kuhitimisha suala hilo”amesema Ndalichako.
Pia amesema kuwa Mtumishi atatakiwa kujaza hati ya ridhaa kwa aliyekuwa mwajiri wak,lakini pia waajiri watawajibika kuwasilisha kwenye mifuko hati za ridhaa pamoja na nyaraka nyingine zinazohusu ulipaji wa mafao kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya mifuko husika.
“Mara baada ya mifuko kupokea nyaraka kutoka kwa aliyekuwa mwajiri malipo yatafanyika kupitia akaunti za benki”amesema.
Vilevile Ndalichako ametoa rai kwa watumishi wote walioondolewa kazini baada ya kubainika kuwa na vyeti vya kughushi wakamilishe taratibu zinazotakiwa ili kuiwezesha mifuko kukamilisha taratibu za kuwarejeshea michango yao.
Lakini pia kwa watumishi ambao tayari wameshafariki stahiki zao watapewa ndugu ambao ndio warithi kupitia mirathi.
“Natoa rai kwa waajiri kuwapa ushirikiano watumishi hao kwa kukamilisha na kuwasilisha mara moja nyaraka zinazotakiwa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii”amesema .
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amesema waajiri wote wanapaswa kuwajibika kwa kutoa ushitikiano kwa watumishi hao iliwa weze kupata nyaraka zao kwa haraka.
“Nawaagiza waajiri wote kuandaa madawati ya msaada ili kuhakikisha zoezi hilo linaenda kwa uharaka zaidi”amesema Mhagama.
Pia amewataka waajiri hao kuzingatia misingi ya utawala bora ikiwemo kuepuka rushwa huku akiitaka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU kuhakikisha hakuna viashiria vyovyote vya rushwa katika zoezi hilo.
Waziri huyo alisema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha jambo hilo la kughushi vyeti halitokei tena kwani vyeti hivyo vitakuwa vinahakikiwa kabla.
“Tumefikia hatua ya juu ya uunganishaji na uoanishaji wa mfumu lakini pia waajiri wanapaswa kuwa makini wakati wa kutoa ajira”amesema
More Stories
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best
Waziri Mavunde:Benki Kuu yanunua tani 2.6 za Dhahabu nchini