Na Allan Kitwe, TimesmajiraOnline, Tabora
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imepongezwa kwa kuipa kipaumbele sekta ya kilimo ili kuleta tija kubwa kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.
Pongezi hizo zimetolewa jana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa Tabora, Neema Kapesa katika hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa Maafisa Ugani wa kata katika manispaa hiyo.
Alisema kuwa Serikali ya awamu ya sita imewapatia vishikwambi na usafiri wa pikipiki ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa weledi mkubwa.
Kapesa alibainisha kuwa jumla ya vishikwambi 21 vimegawiwa kwa Maafisa Ugani wa Kata 21 kati ya 29 zilizopo katika manispaa hiyo ambazo zina Wataalamu wa Kilimo ili kuwarahishia utekelezaji majukumu yao.
“Tunamshukuru sana Rais kwa kutupatia vishikwambi kwa ajili ya Maafisa Ugani wote na hivi karibuni aliwapatia pikipiki 20 kwa ajili ya ufuatiliaji shughuli za wakulima na juzi tumepokea gari jipya 1’, alisema.
Kapesa alitaja vifaa vingine vilivyoletwa na serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa ajili ya kuchochea ufanisi wa sekta hiyo kuwa ni mavazi maalumu ya kazi kwa ajili ya maafisa ugani wote ikiwemo magari mapya 4 ya idara ya afya, elimu na ujenzi.
Akikakidhi vifaa hivyo kwa wahusika Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Ramadhan Kapela alimshukuru sana Rais Samia kwa dhamira yake njema ya kuinua sekta ya kilimo nchini na kuwainua kiuchumi wakulima wote.
Akiongea kwa niaba ya wenzake, Afisa Ugani wa Kata ya Malolo, Shaban Balangula aliishukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kuwajali na kuwawezesha vitendea kazi huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii kubwa.
Alibainisha kuwa awali walikuwa wanashindwa kuwafikia wakulima wote katika maeneo yao kutokana na ukosefu wa usafiri lakini sasa hawana kisingizio chochote cha kushindwa kwenda vijijini kwa kuwa wana usafiri wa uhakika.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato