Na Allan Vicent, TimesmajiraOnline,Kibondo
RAIS wa Samia Suluhu Hassan amepeleka neema kubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma baada ya kupeleka zaidi ya sh. bil 2.9 ili kuboreshwa upatikanaji huduma ya maji safi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Kibondo (KIUWASA) Mhandisi Aidan Ngatomela ,alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake hivi karibuni.
Amesema kuwa katika miaka mitatu2 ya utawala wa Rais Samia, hali ya upatikanaji huduma ya maji safi na salama ya bomba kwa wakazi wa Mji huo imeboreshwa kwa kiasi kikubwa na kupunguza adha iliyokuwepo.
Amebainisha kuwa Rais Samia amewapelekea zaidi ya sh bil 2.9 kwa ajili kuifanyia maboresho makubwa miundombinu ya maji na kutekelezwa miradi mipya zaidi ya 6 ambayo imepelekea upatikanaji huduma ya maji kuongezeka mara dufu.
‘Hali ya upatikanaji huduma ya maji katika Mji wetu wa Kibondo haikuwa shwari hata kidogo, kwani maji yalikuwa yanapatikana mara 1 au 2 kwa wiki nzima, lakini baada ya Rais kuingia madarakani amepunguza sana kilio cha wananchi,” amesema.
Mhandisi Ngatomela ameeleza kuwa kutekelezwa kwa miradi hiyo kumewezesha hali ya upatikanaji huduma ya maji katika Mji huo kuongezeka kutoka asilimia 37.1 ya awali hadi kufikia asilimia 67.6 na inaendelea kuongezeka zaidi.
Aidha idadi ya wateja wanaohudumiwa na KIUWASA imeongezeka kutoka 2,160 hadi kufikia 2,838 na uzalishaji maji umeongezeka kutoka lita za ujazo 2,108,000 kwa siku hadi lita 3,030,000 kwa siku na mtandao wa bomba umefikia km 60.
Amebainisha manufaa mengine yaliyopatikana kutokana na uwepo wa maji kuwa ni kuongeza hali ya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali, kujengwa kwa vyoo na kuboreshwa mazingira ya wafanyakazi wa kwenye vyanzo vya maji.
Mhandisi Ngatomela ametaja miradi iliyotekelezwa kuwa ni mradi wa Twabagondozi uliogharimu zaidi ya sh. mil 330 uliohusisha ujenzi wa kisima, nyumba ya mlinzi, tenki la lita 225,000 na tenki dogo la lita 50,000 na ulazaji bomba lenye urefu wa km 2.3.
Mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 na kumaliza kero ya maji kwa wakazi wa Mji huo hasa wanaoishi katika Mitaa ya Malagarasi, Stendi Mpya, Maduka Saba, Kumwayi na Katunguru A, mradi huu huzalisha lita 320,000 kwa siku.
Mingine ni Mradi wa Uboreshaji Huduma ya Usambazaji Maji Kibondo Mjini awamu ya II ambao umegharimu zaidi ya sh mil 430 na mradi wa kuendeleza visima na kuchimba kisima kirefu Kibondo Mjini uliogharimu zaidi ya sh mil 145.
Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa Kituo cha Kusafisha na Kutibu Maji ya Mto Mgoboka kwa gharama ya sh mil 595, mradi huu umekamilika kwa asilimia 100 na kuongeza ubora wa maji yanayotoka katika chanzo hicho.
Mhandisi Ngatomela amebainisha miradi mingine inayoendelea kutekelezwa kwa fedha za Rais Samia kuwa ni ujenzi wa tenki la lita mil 1.5 na ulazaji bomba (sh mil 400) na Usambazaji Maji Mjini Kibondo awamu ya III (zaidi ya sh mil 600).
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu