Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua Kampeni ya TUTUNZANE MVOMERO 2023-2028 wilayani Mvomero mkoani Morogoro inayohamasisha wafugaji kufanya ufugaji wa kisasa ikiwemo kuwa na maeneo yao ya kulima malisho ili kuondokana na migogoro kati yao na wakulima na watumiaji wengine wa ardhi kila uchao.
Rais Samia amezindua kampeni hiyo mapema wilayani Mvomero mkoani Morogoro leo Agosti 3, 2024.
Wakati akizindua kampeni hiyo Rais Samia alisema mradi huo wa kuhamasisha ufugaji wa kisasa una umuhumu mkubwa kwa wafugaji na jamii inayowazunguka.
“Kampeni hii ni muhimu kwetu kwa sababu inakwenda kuleta amani, kuleta ongezeko la malisho, tija na wafugaji kuweza kukopesheka”, alisema Rais Samia.
Aliongeza kwa kusema kuwa kampeni hiyo itasaidia pia kutunza mazingira na kuepusha athari zake huku akiwataka Wakulima na Wafugaji kuheshimiana kwa sababu wote wanategemeana.
Aidha, Rais Samia alitoa pongezi kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na serikali ya mkoa wa morogoro kwa ubunifu wao huku akiwaahidi kuwa Serikali yake itaendelea kuiunga mkono kampeni hiyo ya mfano hapa nchini.
Alifafanua kuwa sekta za mifugo na kilimo zimeajiri watu wengi nchini, na kwa sababu hiyo ataendelea kuweka msukumo ili kampeni hiyo iweze kuleta mabadiliko na mapinduzi makubwa kwa wafugaji na wakulima ili kuwainua na kuwanufaisha wananchi walio wengi.
Halikadhalika aliwaeleza wafugaji na wakulima kuwa mabadiliko hayaepukiki hivyo ni muhimu wakaunga mkono kampeni hiyo ili waweze kuepukana na migogoro ya kila uchao.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, alimshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake na falsafa yake ya 4R ambayo ndio imepelekea kampeni hiyo kuanzishwa.
Vile vile Mhe. Ulega alitoa shukrani za Wizara yake kwa uongozi wa mkoa na wiaya akisema “Mhe. Rais, napenda pia kuwashukuru Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na Mkuu wa Wilaya ya Mvomero kwa kuhamasisha Kampeni hii inayoakisi maono yako ya 4R – yaani Reconciliation (Maridhiano), Resilience (Ustahimilivu) Reform (Mabadiliko) na Rebuilding (Kujenga Upya), katika kuleta maridhiano baina ya jamii za wafugaji na wakulima”.
Waziri Ulega aliongeza kuwa Kampeni hiyo imefanikiwa kuhamasisha wafugaji na wakulima 825 kushiriki kwa vitendo katika kampeni hii. Jumla ya mashamba ya wafugaji 365 yamepimwa na kutengenezewa hati, na miundomibu ya maji kwa wafugaji imejengwa ikiwemo visima sita (6).
Vilevile, jumla ya tani 10 za mbegu za Juncao, kilo 462 za mbegu za Rhodes na miche 10,000 ya miti ya malisho aina ya Leucaena zimegaiwa kwa wananchi ambao ni wanufaika Kampeni hii.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa