
Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema anamrudisha kwa Mama Mbunge wa Jimbo la Bumbuli January Makamba, kwani kilichotokea ni sawa na Mama kumuonya mwanawe.
Ameyasena hayo Februari 24,2025 wakati anahutubia wananchi wa Wilaya ya Lushoto kwenye Uwanja wa CCM wa Sabasaba mjini Lushoto. Ni baada ya Mbunge huyo kutoa neno la shukrani kwa Rais Samia, namna alivyomtendea akiwa Waziri wa Nishati, na baadae Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, lakini pia huduma za jamii na maendeleo kwenye jimbo lake.
“Sisi wamama mnatujua, mtoto akikukera unampiga kikofi na kumfichia chakula, si ndiyo. Sasa mwanangu (January) nilimpiga kikofi nikamfichia chakula, lakini leo namrudisha kwa Mama” alisema Rais Dkt. Samia na kumwita January na kumkumbatia.
Rais Dkt. Samia alisema amefungua Jengo la Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli (Bumbuli DC) ambalo litahudumia wananchi wote, hivyo amewataka kulinda miundombinu na vifaa vyake., huku wakitoa huduma nzuri kwa wananchi.
“Madhumuni ya jengo lile ni kusogeza huduma kwa wananchi, na huduma zote za halmashauri ziwe kwenye jengo moja, na lengo kubwa kabisa ni kudumisha au kuimarisha Utawala Bora, hivyo wananchi wa Bumbuli hongereni sana kwa jengo lile sababu ni zuri, litumieni kwa huduma mnazozitaka.
“Lakini pia jengo lile litunzeni. Wafanyakazi waliopo ndani ya jengo hili nataka huduma zinazotolewa kwa ndani pia ziwe nzuri. Sio jengo lina viyoyozi, lakini huduma kwa wananchi hakuna, hiyo hapana” alisema Dkt. Samia.
Dkt.Samia alisema katika kipindi cha miaka minne halmashauri 122 zimepata majengo mapya na mazuri, na kuongeza kuwa kama wabunge wwatatu wa wilaya ya Lushoto walivyosema, huduma za jamii ikiwemo maji, umeme, elimu, barabara vimewafikia wananchi.

Naye Makamba alisema anamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuweza kuwaondolea kilio cha zaidi ya miaka 20 cha barabara ya Soni- Bumbuli- Dindira- Kwashemshi- Old Korogwe, ambapo tayari mipango ya kuweka lami inafanyika.
“Sisi watu wa Bumbuli kwa muda mrefu sana tumekuwa tunazungumzia barabara ya Soni- Bumbuli- Dindira- Kwashemshi na Korogwe, kwa miaka 20 sasa imekuwa ndiyo kilio chetu Juzi karibu wiki tatu zilizopita tumepata taarifa ya Waziri wa Ujenzi kuwa wewe Waziri kuwa umetoa kibali sasa kwamba barabara hiyo itangazwe na kujengwa ujenzi kwa kiwango la lami.
“Mheshimiwa Rais utakuwa umeacha historia kubwa sana katika Milima hii ya Usambara. Kama unavyofahamu, barabara ya Lushoto ni moja, na sasa tutakuwa na barabara mbili, kwani huko nyuma mvua zilinyesha kukatokea maporomoko ya mawe (Soni- Mombo), na kufanya barabara ishindwe kupitika kwa wiki mbili, na kufanya vitu vipande bei, hivyo barabara hii itatoa fursa za kiuchumi kwa wananchi na wakulima wetu” alisema Makamba.
Makamba amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa kumteua kuwa Waziri. Kwanza Waziri wa Nishati na baadae Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, hiyo kwake ni historia na haitafutika kwenye maisha yake hadi atakapoingia kaburini
“Naomba nishukuru sana kutoka sakafu ya moyo wangu kwa kuniamini mimi, kwanza kwa kuniteua kuwa Waziri wa Nishati, na baadae Waziri wa Mambo ya Nje. Ni heshima kubwa ambayo haitafutika katika uhai wa maisha yangu. Katika kipindi nimefanya kazi na wewe nimejifunza sana, na nimeerevuka sana kutokana na uongozi wako.
“Lakini kabla ya hapo nilikuwa Waziri wa Nchi (Muungano na Mazingira) katika ofisi yako, na wewe ndiyo umenifundisha kazi, sababu tulifanya kazi wote miaka minne, na hiyo ilikuwa nafasi yangu ya kwanza ya uwaziri. Kama nina uerevu nilionao kwenye utumishi wa uwaziri, basi umetokana na mkono wako Mheshimiwa Rais naomba nikushukuru, na hii nitaenda nayo kaburini kwangu” alisema Makamba.

More Stories
Kikwete kufuatilia mchakato ujenzi wa barabara Mbalizi-Makongolosi
Exim bank yaingia mkataba wa Zati
Milioni 236 kunufaisha vikundi 17 vya wanawake Minazi Mirefu