September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

‘Rais Samia ameridhia wananchi kuwa kitovu cha maendeleo’

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Tarime

WAZRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuwafanya wananchi kuwa kitovu cha maendeleo kwa kuhakikisha wanakuwa na fikra chanya katika maendeleo, yenye maadili mema, malezi na makuzi chanya ya watoto, jamii isiyo na ukatili wa kijinsia, yenye uzalendo kwa nchi yao.

Waziri Dkt. Gwajima aliyasema hayo juzi wilayani Tarime mkoani Mara wakati wa ziara ya kuhamasisha jamii kupambana na vitendo vya ukatili.

Waziri Dkt. Gwajima alisema lengo la Wizara yake ni kuhakikisha jamii inaelimika kimaendeleo kwa inayofanya kazi kwa bidii na kujitoa, kujali na kuhifadhi rasilimali za nchi, kuwa na lishe na afya bora, matumizi sahihi ya TEHAMA, jamii inayojiwekea akiba, jamii yenye uwezo wa kuzitambua na kuzitatua changamoto zao kwa kushirikiana na Serikali.

Alieleza jamii isiyo na ukatili inakuwa na mazingira mazuri ya kufanya shughuli za maendeleo hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu na fursa ili jamii iweze kujiwamua kiuchumi na kupambana na vitendo vya ukatili.

“Natoa rai kwa viongozi, wataalamu wa Maendeleo ya jamii na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kujenga mazingira rafiki ili kuwasaidia wananchi kufanya shughuli za maendeleo bila hofu wala woga dhidi ya vitendo vya ukatili.” alisema Waziri Dkt. Gwajima.

Alisema katika kuhakikisha jamii inakuwa na ustawi, Serikali kwa kushirikiana na wadau inatekeleza afua zinazolenga kumaliza changamoto zinazosababisha ukatili zikiwemo kuimarisha uchumi wa kaya kwa kuendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu, kutoa elimu kuhusiana na mila na desturi zenye madhara na kuimarisha mila zenye matokeo chanya.

Alizitaja afua nyingine kuwa ni kuimarisha ulinzi wa mwanamke na mtoto katika maeneo ya umma na katika mitandao, kuongeza vituo vya kutolea huduma kwa wahanga wa ukatili kama vile nyumba salama na vituo vya mkono kwa mkono na kwa kiwango kikubwa kushirikisha wanaume katika kutokomeza vitendo vya ukatili.

Aliupongeza mkoa wa Mara kwa ujumla kwa jitihada za kutokomeza ukatili wa kijinisa ambapo kwa mujibu wa utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS) kwa mwaka 2015/2016, ukeketaji umepungua kutoka asilimia 32 (2016) hadi 28 (2022), huku vitendo hivyo vikiongoza katika mikoa ya Arusha (asilimia 43) na Manyara (asilimia 43).

Aidha, Waziri Dkt. Gwajima aliwapongeza wananchi wa Kata ya Ganganye kwa kuonesha uzalendo katika masuala ya kimaendeleo na kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ukatili wa kijinsia, amesema jamii ndio sehemu pekee katika kuhakikisha wanaondokana na vitendo vya ukatili.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tarime Meja Edward Gohele alisema wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kufikisha elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili ili jamii iondokane na vitendo hivyo na kujikita katika shughuli za maendeleo katika maeneo yao.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini Yassin Ali amesema Shirika hilo linashirikiana na Serikali katika kuhakikisha inafikia Jamii kutoa elimu na kuhamasisha kupambana na vitendo vya ukatili katika maeneo yao.

“Mhe. Waziri katika kupambana na vitendo vya ukatili sisi Shirika la Kivulini tumekuja na mbinu za kutumia ushabiki wa Mpira kwa timu za Simba na Yanga ili kuishirikisha Jamii katika kupambana na vitendo vya ukatili,” alisema Ali.

Mwishooooooooooooooooooooo