Na Yusuph Mussa, Tanga
RAIS wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi kwa kuweka miundombinu mbalimbali ikiwemo kuboresha bandari, viwanja vya ndege, barabara, reli, umeme na maji ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Rais anafanya hivyo sababu, ili nchi iweze kuwa na uchumi imara na endelevu, ni lazima Sekta Binafsi iwe na nguvu, na kwa Tanzania Sekta Binafsi inaajiri watu kwa asilimia 95 wakati Serikali inaajiri kwa asilimia tano.
Hayo yamesemwa Novemba 16, 2023 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji) Profesa Kitila Mkumbo wakati anafungua Kongamano la Uwekezaji, Biashara na Utalii, na Uzinduzi wa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Tanga, huku kauli mbiu ikiwa ni ‘Wekeza Tanga kwa uwekezaji endelevu’ lililofanyika jijini Tanga.
“Rais Dkt. Samia alipokuwa Nairobi alisema nakwenda kuifungua nchi. Watu wengi hawakumuelewa, lakini aliposema kufungua nchi ni kuimarisha uchumi kwa kuimarisha Sekta Binafsi na kuwavutia wawekezaji. Serikali haifanyi biashara wala kuajiri watu. Kazi ya kufanya biashara ama kuajiri watu ni ya Sekta Binafsi ikiwemo wawekezaji.
“Hivyo, Serikali haitengenezi ajira, bali inaweka mazingira mazuri ya kufanya biashara na uwekezaji. Katika ajira 100 Tanzania, ajira 95 zinatolewa na Sekta Binafsi, na Serikali inatoa ajira tano tu. Na ili kuvutia uwekezaji katika Sekta Binafsi, kazi ya Serikali ni kujenga miundombinu na mazingira wezeshi, na kazi hiyo imefanywa na Rais Dkt. Samia kwa kujenga miundombinu ya bandari, barabara, umeme, upatikanaji wa maji, na uboreshaji huduma za jamii” amesema Profesa Mkumbo.
Profesa Mkumbo amesema tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1961, maadui watatu wa Taifa walikuwa ujinga, maradhi na umasikini, lakini maadui wa sasa ni watu wanaokwamisha uchumi wa Tanzania kukua kwa kuwawekea vikwazo vingi wawekezaji.
“Moja ya vikwazo vitatu vya uchumi ni udhibiti uliopitiliza kwenye uwekezaji. Na Rais Dkt. Samia anataka kubomoa mnyororo unaokwanza Sekta Binafsi. Lugha sasa sio kudhibiti bali kuwezesha. Afisa Biashara ukimkuta mfanyabiashara hana leseni, afanye kazi ya kumsaidia apate leseni. Afisa Biashara anaetutia umasikini ni yule anaemkuta mfanyabiashara ambaye hana leseni, na kumueleza leo utanikoma, funga biashara yako.
“Askari wa usalama barabarani wanaosimamisha malori nchi nzima kila mahali, wanatutia umasikini. Hata sisi mawaziri tuna suti nzuri na magari mazuri ni sababu wafanyabiashara wanalipa kodi. Hata askari anaposimamisha lori, ajue nguvu ya kuinua mkono anaipata sababu ya kodi ya wafanyabiashara, hivyo tuondoe urasimu kwa wafanyabiashara na wawekezaji” amesema Profesa Mkumbo.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema alipokwenda Tanga alitaka kuchachua uchumi wa Tanga, kwani Mkoa wa Tanga ndiyo ulikuwa unaongoza kwa kuchangia Pato la Taifa (GDP) kutokana na zao la mkonge, hivyo amedhamiria kwa kuhakikisha Tanga inafunguka kwa fursa mbalimbali.
“Nilipokuja, niliamua kuifungua Tanga. Wote ni mashahidi, Tanga kuna fursa nyingi za kiuchumi ikiwemo Bomba la Mafuta ambapo uwekezaji wake ni dola za Marekani bilioni 4. 4, uwekezaji wa Bandari ya Tanga umefanyika kwa sh. bil. 429.1. Sasa kina cha maji ni mita 13 kutoka mita tatu. Tanga tuna kilimo cha mkonge, chai, viungo, mahindi, korosho, alizeti na mbogamboga na matunda.
“Tuna Uchumi wa Buluu. Samaki Tanga ni wengi tukiwa sambamba na Wilaya ya Kilwa. Tuna Boti yenye uwezo wa kubeba watu 615 kwa safari za Tanga- Unguja- Pemba. Tunawaeleza watu wa mikoa ya Kaskazini, sasa mtatumia boti kutoka Tanga kwenda Unguja, na sio lazima tena waende Dar es Salaam.
Nawahakikishia wafanyabiashara kuwa mizigo yenu inayopita Tanga ipo salama, na nawahakikishia ulinzi na usalama” amesema Kindamba.
Kindamba amesema wanamshukuru Rais Dkt. Samia kwa kuifungua barabara za Pangani- Saadan- Bagamoyo kwa kujengwa kwa kiwango cha lami, kwani kunaifanya Tanga kufikika na kutoka kwa njia ya bahari, ndege, reli na barabara, hivyo kufanya wawekezaji kupata urahisi wa kufanya shughuli zao.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa