Na Mwandishi Wetu,TimesMajiraOnline,Dar
MWAKA mpya wa 2023 umekuwa wa kihistoria kwa wanasiasa nchini kufuatia Rais Samia Suluhu Hassan kutangaza kufuta zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa lililotangazwa mwaka 2016 na Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.
Rais Samia alitangaza kufuta zuio hilo alipozungumza na viongozi wa vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu, Ikulu, jijini Dar es Salaam, mwanzoni mwa mwezi huu.
“Mikutano ya vyama vya siasa ni haki ya vyama vya siasa. Uwepo wangu hapa leo ni kuja kutangaza kuwa lile tangazo la kuzuia mikutano ya hadhara sasa linaondoshwa,” alisema Rais Samia na kushangiliwa na viongozi wa vyaa vya siasa.
Alisema kwa upande wa Serikali wajibu wetu ni kulinda mikutano ya vyama vya siasa, mnachotakiwa ni kutoa taarifa Polisi na kwa hatua tuliyofikia wajibu wetu ni kuwalinda hadi mnamaliza mikutano yenu salama.
“Lakini wajibu wenu vyama vya siasa nikufuata sheria na kanuni zinavyosema na kama Watanzania tunatoa ruhusa za mikutano ya vyama vya siasa tukafanye siasa za kujenga na sio kubomoa. Tukafanye siasa za kistaarabu. Sisi ndani ya CCM tunaamini kukosoa na kukosolewa.”
Uamuzi huo umezidi kufungua ukurasa wa maridhiano ambalo limekuwa hitaji kubwa la Rais Samia tangu alipoingia madaraka. Miongoni mwa kauli zake za kwanza alizotoa mara baada ya kuapishwa ni kuwataka Watanzania wasitazame mbele kwa mashaka na badala yake wasahau yaliyopita.
Hatua ya Rais Samia kufuta zuio la mikutano ya wanasiasa ni wazi amewezesha wanasiasa kusahau yaliyopita. Hatua hiyo pia imewezesha wanasiasa waliokimbilia nje uhamishoni tangu uchaguzi wa 2020 kutangaza kurudi nchini.
Miongoni mwa wanasiasa hayo ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ambaye ametangaza kurudi nchini Januari 25. Kiongozi huyo wa upinzani nchini atarejea nchini akitokea uhamishoni, nchini Ubelgiji na kuahidi kufungua ukurasa mpya.
Lissu anarejea nyumbani baada ya Rais Samia kuondoa zuio la mikutano ya kisiasa lililowekwa na mtangulizi wake hayati John Magufuli.
Lissu anasema kwamba hawana sababu ya kuendelea kuishi uhamishoni na kuongeza kuwa ana uhakika wataandika ukurasa mpya mwaka huu wa 2023 ambao ametabiri utashuhudia mabadiliko makubwa ya kihistoria nchini
Lissu ambaye alipigwa risasi mara 16 katika jaribio la kumuua la mwaka 2017, amekuwa akiishi nchini Ubelgiji akihofia usalama wake na ameahidi kurejea nyumbani Januari 25.
Kwa mara ya mwisho Lissu alikuja nchini mwaka 2020 kwa ajili ya kugombea nafasi ya urais akichuana vikali na Magufuli.
Mbali na Lissu, wanasiasa wengine waliokimbilia uhamishoni ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na aliyekuwa mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje.
Kwenye hotuba yake ya mwaka mpya miongoni mwa mambo ambayo alisisitiza Lissu ni kurejea nchini Januari 25, mwaka huu akitokea nchini Ubelgiji alikokimbilia.
Alisema licha ya ahadi ya Rais Samia na utayari wake (Lissu) na chama chake wa kufanya siasa, siku zijazo hazitakuwa rahisi kwao.
“Ninajua tutakabiliwa na majaribu ya kila aina na tutapitishwa katika tanuru kubwa la matatizo na magumu mengi.
“Lakini licha ya mazingira hayo magumu na mbele ya changamoto kubwa na nyingi zitakazotukabili, ninaamini kwamba kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Yeremia, Mwenyezi Mungu anatuwazia sisi Watanzania mawazo ya kutustawisha na wala sio ya kutuumiza, mawazo ya kutupa tumaini kwa siku zetu zijazo,” alisema Lissu.
Lissu, alisema amelazimika kuchewa kutoa salam za mwaka mpya kutokana na kikao cha Rais Samia na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema 2023 ni wa kupambana kupata Katiba mpya.
“Ni mwaka ambao kama tukiamua kwa dhati ya mioyo yetu, tutapata Katiba mpya na ya kidemokrasia, yenye mfumo huru wa uchaguzi, inayojali na kulinda haki za wananchi na inayoweka misingi imara ya uwajibikaji wa viongozi wetu kwa wananchi na wawakilishi wao,” alisema.
Anasema kwa kuwa Rais Samia na chama na Serikali wameshaahidi hadharani kwamba wako tayari kuanza safari hiyo ndefu na ngumu, wako tayari kumjibu kwa vitendo kwamba wamejipanga kwa safari hiyo.
“Mimi binafsi na chama chetu tuko tayari na tumejiandaa kwa safari hiyo. Ninarudi kwa ajili ya kazi kubwa iliyoko mbele yetu, kazi ya Katiba mpya na mwanzo mpya kwa Taifa letu,” alisema Makamu Mwenyekiti huyo.
Anasema kutokana na mwelekeo uliotolewa na Rais Samia kuhusu mabadiliko makubwa ya kisheria na kikatiba yanayohitajika kufanyika kama sehemu ya maridhiano ya kisiasa nchini, bado kuna kazi kubwa ya maandalizi ya kitaalamu na timu za wataalamu wa Chadema, CCM na Serikali.
Lissu, aliondoka nchini Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi jijini Dodoma, anasema miaka mitano ya kuishi uhamishoni imekuwa ya mateso.
Lissu, aliyekwenda kutibiwa Nairobi nchini Kenya kabla ya kuhamishiwa nchini Ubelgiji, alirejea nchini Julai, mwaka 2020 kushiriki Uchaguzi Mkuu na aliondoka tena kurejea Ubelgiji Novemba 2020.
“Ukiondoa takriban miezi mitatu ya kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020, nimeishi uhamishoni kwa zaidi ya miaka mitano.
“Hiki kimekuwa kipindi kirefu na kigumu sana katika maisha yangu binafsi na yetu kama chama na kama Taifa. Hata hivyo, kama nilivyosema katika salamu zangu za mwaka mpya mwaka jana, “hatuwezi kuendelea kuishi uhamishoni bila ukomo,” alisema Lissu.
Alisema anatarajia kurejea nchini Januari 25 na atatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Ethiopia akitokea Brussels, Ubelgiji, kupitia Addis Ababa, Ethiopia.
“Panapo majaliwa nitakanyaga udongo wa ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena siku ya Jumatano ya tarehe 25 Januari, 2023, majira ya saa saba na dakika 35 mchana.
“Kwa vyovyote itakavyokuwa, mwaka huu utakuwa wa muhimu sana katika historia ya nchi yetu. Tukiweka nia ya dhati na kuitekeleza kwa dhati, tutayashinda majaribu na magumu yaliyo mbele ya safari yetu,” alisema.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia