Na Allan Vicent, TimesmajiraOnline,Tabora
MIAKA mitatu ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan madarakani imeleta neema kubwa kwa wakulima wa zao la tumbaku Mkoani Tabora baada ya Makampuni yaliyopewa dhamana kununua tumbaku yote inayolimwa na wakulima.
Wakulima wameeleza kufurahishwa na hatua ya Makampuni hayo kutoweka kikwazo cha kununua kwa makisio ya awali pekee kama ilivyokuwa huko nyuma, hali ambayo imeongeza hamasa kwa wakulima wengi zaidi kulima zao hilo.
Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti wakazi wa Kijiji cha Msange, Kata ya Kalunde katika halmashauri ya manispaa Tabora wamesema kuwa zao hilo sasa ni kimbilio la wakulima kutokana na manufaa wanayopata.
Mkazi wa Kijiji hicho Subira Salumu ambaye ni mkulima na Katibu (Meneja) wa Chama Cha Msingi Twende Pamoja anasema kuwa awali chama chao kilikuwa na wakulima 25, lakini sasa wameongezeka hadi kufikia 392 ndani ya miaka miwili.
Anaeleza kuwa katika kipindi cha miaka mwili kilimo cha tumbaku kimeleta tija kubwa kwa wakazi wa kijiji hicho na vijiji vingine baada ya kutatuliwa changamoto zilizokuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu ikiwemo kucheleweshwa pembejeo.
‘Msimu uliopita tulikisia kuzalisha kilo 500,000 lakini tukazalisha kilo 520,000 na zote zikanunuliwa na Kampuni ya Alliance One, baada ya kuuza tulipata zaidi ya sh bil 2.4, na kila mkulima alipata fedha zake taslimu pasipo kukopwa’, alisema.
Mwenyekiti wa Chama hicho Ramadhan Mohamed anaishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kujali wakulima na kuwarahisishia upatikanaji wa pembejeo na masoko, sasa hivi hakuna usumbufu tena, kiasi chochote kinachozalishwa kinanunuliwa.
Anaongeza kuwa maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali ya Rais Samia katika sekta ya kilimo yamewezesha wakulima wa zao hilo katika kijiji hicho na maeneo mengine kupata manufaa makubwa ikiwemo kujenga nyumba za kisasa, kununua vyombo vya usafiri na kusomesha watoto wao.
Chiku Rajabu mkulima mkazi wa Kata ya Kalunde katika manispaa hiyo anasema kuwa tangu aanze kulima zao hilo zaidi ya miaka 10 iliyopita walikuwa hawana masoko ya uhakika na walikuwa wanapewa ukomo wa kilo za kuzalisha lakini sasa hakuna ukomo.
“Tunamshukuru sana mama yetu Rais Samia kwa kutuletea wanunuzi wa kutosha na ruzuku ya mbolea, sasa hivi tunauza bei nzuri, mwaka jana nililima ekari nne nikavuna kilo 5600 ambapo nilipata zaidi ya sh mil 23, si haba’, alisema.
Anatoa wito kwa wanawake wenzake kuchangamkia fursa za kilimo hasa kilimo cha zao hilo ili kujikwamua kiuchumi, na kusisitiza kuwa kilimo kinalipa wasikae nyumbani na kusubiri kuletewa kila kitu na waume zao.
Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Kalunde Sizya Kagoma alimpongeza Rais Samia kwa kusikia kero ya wakulima na kuwaondolea vikwazo vilivyokuwa vikiwarudisha nyuma kiuchumi, sasa wanafurahia serikali yao.
Anashauri makampuni yote yaliyopewa dhamana ya kununua tumbaku ya wakulima katika Mkoa huo kuhakikisha yanajipanga vizuri katika kipindi hiki cha msimu wa mavumo ili masoko yatakapoanza kila mkulima apate stahiki yake.
Naye Afisa Ugani wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Mkoani Tabora (WETCU) Michael Zakaria alisema kuwa hadi sasa jumla ya makampuni 7 yameruhusiwa na serikali kununua zao hilo Mkoani hapa.
Anataja baadhi ya makampuni hayo kuwa ni Alliance One, Japan Tobacco International (JTI), Mkwawa Tobacco Leaf, Vodi cel, Magefa na nyinginezo.
Lucy Kasebuye (40) mkulima mkazi wa Ibelamilundi anamshukuru Rais Samia kwa kuboresha mazingira ya upatikanaji pembejeo za kilimo kwa wakati hali iliyochochea wananchi wengi kulima zao hilo kwa kiwango kikubwa.
Anabainisha kuwa tangu ameanza kulima zao hilo miaka 7 iliyopata hakupata mafanikio makubwa, lakini tangu Rais Samia aingie madarakani wakulima wa tumbaku wamekuwa mamilionea na wanasomesha watoto hadi vyuo vikuu.
Anasisitiza kuwa chama chao cha msingi Ibelamilundi AMCOS chenye wanachama 180 kilikuwa kimedorora kutokana na uhaba wa masoko ya kuuzia tumbaku yao, lakini sasa yamekuja makampuni mengi na kuongeza ushindani wa bei nzuri.
‘Nina watoto sita, wawili wanasoma shule ya msingi, wawili sekondari na wengine wawili sasa hivi wapo Chuo Kikuu cha SAUT Mbeya, nawasomesha kupitia zao hili hili na nimejenga nyumba nzuri, tunamshukuru sana Rais Samia,” anasema.
Hussein Ramadhani (50) mkulima Mkazi wa Kijiji cha Igoko, kata ya Isikizya anaeleza kuwa awali alikuwa analima ekari moja, lakini sasa analima ekari 4 na zaidi za tumbaku, mwaka jana alivuna kilo 4500 na kupata zaidi ya sh mil 23 na msimu huu amelima ekari 5, matarajio ni kupata kilo 6000 na atauza zaidi ya sh mil 35.
‘Kwangu zao la tumbaku ni dhahabu, imenipa manufaa makubwa sana, nimejenga nyumba ya kisasa hapa hapa kijijini, nimenunua mifugo, nasomesha watoto na msimu ujao baada ya kuuza nimepanga kununua gari,” anasema.
Diwani wa Kata ya Ibelamilundi, Ferdinand Magazi anamshukuru Rais Samia, Waziri wa Kilimo Hussien Bashe na Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini Almas Maige kwa kusimamia vizuri kilimo cha tumbaku, sasa limekuwa lulu.
Alibainisha kuwa wakulima wa zao hilo walikuwa wameanza kupoteza mwelekeo na wengine walishakata tamaa na kufikilia kuachana nalo lakini sasa serikali ya awamu ya 6 imeleta neema, sasa kila mwanakijiji anatamani kulima tumbaku.
Salumu Sudi (52) mkulima, mkazi wa Kijiji cha Nzigala kata ya Kigwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Msingi Kigwa Kijiji alisema kuwa wakulima wote sasa hivi wanafurahia zao hilo kutokana na masoko ya uhakika yaliyopo.
Anabainisha kuwa makampuni yote yanayonunua zao hilo yameajiri Maafisa Ugani na kuwasambaza katika Vijiji vyote ili kutoa elimu ya kilimo bora kwa wakulima, hali hii imeongeza uzalishaji wa zao hilo kila msimu na wakulima kunufaika zaidi.
Anatoa wito kwa wakulima wote kuendelea kufuata maelekezo ya wataalamu ili kuzalisha tumbaku yenye ubora unaotakiwa hivyo kujiongezea kipato zaidi na kujikwamua kiuchumi.
More Stories
Siri ya Rais Samia kutembea kifua mbelea kijivunia Mapinduzi Matukufu ya Z,bar
Rais Samia anavyotimiza ahadi yake ya kumtua ndoo ya maji mwanamke
Rais Samia anavyozidi kusogeza karibu watoto wa kike na kasi ukuaji teknolojia