December 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia alakiwa kwa Shangwe,akianza ziara Ruvuma

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),, amewasili Mkoa wa Ruvuma na kupokelewa kwa nderemo na vifijo, wakati akianza ziara ya kikazi mkoani humo, leo Septemba 23, 2024.

Wananchi wa Mji wa Songea, wakiongozwa na viongozi wa Chama na Serikali, walijitokeza kwa wingi kumpokea Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, katika Uwanja wa Ndege wa Songea, kwa shangwe na vigelegele.

Baada ya kuwasili uwanjani hapo, Rais Samia Suluhu Hassan, alipata fursa ya kukagua na kupewa taarifa ya ukarabati na maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Songea, kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Ndugu Innocent Bashungwa na watalaam kutoka wizarani.

Rais Samia kabla ya kuondoka uwanjani hapo kuendelea na ratiba za shughuli nyingine katika siku ya kwanza ya ziara yake katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Ruvuma, pia amepata fursa ya kutazama vikundi mbalimbali vya burudani, vikiongozwa na vikundi vya ngoma za asili za Mkoa wa Ruvuma.

Baadae leo jioni, Rais Samia anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Tamasha la 3 la Kitaifa la Utamaduni, ambalo mwaka huu limefanyika mkoani Ruvuma.