January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aibeba sekta ya utalii Tanzania, yang’ara Barani Afrika


Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KAZI kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kuitangaza seta ya utalii imewezesha Tanzania kushika nafasi ya pili kwenye orodha ya Nchi za Afrika zilizofanya vizuri kwenye utalii katika robo ya kwanza ya mwaka 2023.

Tanzania imetangazwa kushika nafasi ya pili kwa utalii bora Afrika katika Mkutano wa Dunia kuhusu Utalii Kanda ya Afrika uliofanyika Mauritius.

Katibu Mkuu wa Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa Kanda ya Afrika (UNWTO-CAF) Zurab Pololikashshvilia, alitangaza Tanzania kushika nafasi ya pili wakati akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa mpango kazi wa Shirika hilo kwenye kikao kazi cha mkutano wa 66 kilichofanyika Mauritius.

Alisema nchi ya kwanza ni Ethiopia, huku Morocco ikishika nafasi a tatu. Ushindi huo wa Tanzania ilithibitishwa na Katibu Mku Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, akisema Tanzania imeshika nafasi ya pili kwa kupata watalii wengi zaidi Afrika kwa robo ya kwanza ya mwaka kuanzia Januari hadi Machi 2023.

Kwa mujibu wa Dkt. Abbas kwa kipindi hicho, Tanzania ilipata zaidi ya watalii 800,000 ikilinganishwa na watalii 200,000 kwa mwaka 2022 kwa kipindi hicho cha robo mwaka

Mbali na Tanzania kushika nafasi ya pili, mapato yatokanayo na shughuli za utalii nchini zinazosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa robo ya kwanza ya mwaka 2023 nayo yaliongezeka.

Kwa mujibu wa taarifa ya Takwimu za Utalii kwa robo ya mwaka kuanzia Januari hadi Machi 2023 shughuli za utalii nchini ziliingiza takribani kiasi cha sh. bilioni 116.5 ikilinganishwa na sh. bilioni 65.0 zilizoingizwa kipindi kama hicho mwaka 2022.

Hii inamaanisha kwamba, kwa robo ya kwanza ya mwaka 2023, shughuli za utalii nchini zinazosimamiwa na Wizara, mapato yake yaliongezeka kwa takribani sh. bilioni 51.5 sawa na ongezeko la asilimia 231.8.

Mwezi wa Januari na Februari wa robo ya kwanza ya mwaka 2023 ilikuwa na ongezeko sawa la mapato ya takribani asilimia 95.0 ukilinganisha na ya robo ya kwanza ya mwaka 2022. Hiyo ni kwa Mbali na mapato hayo.

Aidha, Sekta ya Maliasili na utalii inachangia pato la taifa kwa asilimia 17.5 na fedha za kigeni asilimia 25,pamoja na kutoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja.

Mafanikio hayo ya Tanzania kushika nafasi ya pili kwa utalii bora Afrika na kuongezeka kwa mapato ya shughuli zitokana na utalii ni kielelezo cha juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, kutokana na kazi kubwa za kuitangaza nchi yetu kimataifa kupitia programu ya
Tanzania – The Royal Tour.

Programu hiyo imewezesha kuitambulisha Tanzania kimataifa kwa kutangaza vivutio vya utalii vya kipekee vya nchi yetu, kuonesha fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye sekta ya maliasili na utalii pamoja na kuimarisha nafasi ya nchi katika Jumuiya za kimataifa.

Kimsingi, programu hii imehusisha uandaaji wa filamu inayoonesha vivutio na fursa za uwekezaji zilizopo nchini. Pamoja na maeneo mengine, filamu hiyo inaonesha pia vivutio mbalimbali vya utalii katika hifadhi za Taifa, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro,
maeneo ya malikale, tamaduni zetu na visiwa vya Zanzibar.

Programu hii ilizinduliwa Aprili, 2022 katika Jiji la New York na Jiji la Los Angeles nchini Marekani; na kuendelea katika Jiji la
Arusha, Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar.

Katika uzinduzi wa filamu hiyo uliofanyika nchini Marekani, zaidi ya watu 6,000 walishiriki wakiwemo viongozi wa kitaifa, viongozi wa majiji husika, watu maarufu, wadau wa utalii na uhifadhi, wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali.

Uzinduzi huo pia ulishirikisha vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa vikiwemo, vituo vya televisheni na redio vya
CBS, Fox News, NBC, YouTube na PBS – Amazon Prime video.

Programu ya Tanzania – The Royal Tour imezaa matunda kwa kuvutia
watalii na wawekezaji mbalimbali kutembelea nchini.

Mathalan, wakala wa utalii zaidi ya 30 kutoka katika masoko ya utalii yakiwemo Marekani, Ufaransa na Lithuania wamehamasika kutembelea nchini ili kujifunza na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii kwa lengo la kuvitangaza katika nchi zao.

Aidha, wawekezaji kutoka Taifa la Bulgaria wameonesha nia
ya kuwekeza nchini kwa kujenga hoteli nne zenye hadhi ya nyota tano katika hifadhi za Taifa Serengeti, Ziwa Manyara na Tarangire; na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Katika hatua nyingine, Serikali imesaini mkataba wa ushirikiano katika masuala ya utalii, biashara na uwekezaji baina ya
Tanzania na Jiji la Dallas Marekani, mwezi Aprili, 2022.

Hatua hiyo itafungua fursa za usafiri wa anga kwa kuwezesha safari za moja kwa moja za ndege kutoka Tanzania hadi Dallas, Marekani na hivyo kuongeza idadi ya wageni nchini.

Sambamba na hilo, mtandao maarufu wa habari nchini Marekani
ujulikanao kama theGrio umetambua juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuiongoza vyema sekta ya utalii na uhifadhi nchini.

Jitihada hizo za Rais Samia zimeleta matokeo chanya katika kuongeza idadi ya watalii na hivyo kufikia lengo la watalii milioni 5 na mapato Dola za Marekani bilioni 6 ifikapo mwaka
2025, kama ilivyoelekezwa katika Ibara 67(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020 – 2025