May 3, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia afanya ziara ya kushtukiza daraja la Tanzanite

Na Mwandishi wetu,timesmajira,online

RAIS  wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan  amefanya ziara ya kushtukiza kukagua maendeleo ya ujenzi wa daraja la Tanzanite linalojengwa katika eneo la Selander Jijini Dar es Salaam.

Rais Samia amepokea maelezo ya ujenzi wa daraja hilo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini TANROADS Mhandisi Rogatius Mativilla ambaye amesema ujenzi wa daraja hilo umefikia asilimia 70.

Mhandisi Mativila amesema daraja hilo litakapokamilika litapunguza msongamano wa magari,  ajali bararani, litaboresha hali ya maisha Jijini  Dar es Salaam pamoja na kupendezesha jiji la Dar es Salaam na kuwa sehemu moja wapo ya kivutio cha utalii katika fukwe zilizopo karibu na daraja hilo.

Wakati huohuo,Rais Samia  amefanya ziara katika eneo la Coco Beach ili kuona agizo lake la kutaka wafanyabiashara wadogowadogo kupangwa vizuri katika mazingira bora ya kufanya biashara linavyoendelea kutekelezwa.

Aidha, Rais amesema ziara hiyo pia imemuwezesha kuona hali halisi ya athari za mabadiliko ya tabianchi katika fukwe za Coco beach na kusema kuwa Serikali itaangalia upya namna ya kuzuia athari hizo.

Rais Samia amesema kuwa Serikali itaendelea kuwajali wafanyabiashara wadogo wadogo na kutolea mfano eneo hilo ambalo wafanyabiashara wakubwa walilitaka lakini Serikali ilikataa kwa kujali maslahi ya wafanyabiashara wadogo ili waendelee kukuwa na kujipatia kipato.

Pia, Rais amesema Serikali kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imetenga kiasi cha Sh. Bilioni 5 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyabiashara wadogo ambao itabidi kuzirejesha ili kuwezesha wengine kupata mikopo hiyo na kuendeleza biashara zao.

Rais Samia amesema zoezi la lengo la kuwapanga wafanyabiashara wadogo wadogo mijini ni zuri ambalo limelenga kuwaboreshea mazingira yao ya biashara, kuweka miji katika hali ya usafi pamoja na kuimarisha usalama.

Vilevile,Rais Samia ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango Pamoja na TAMISEMI kuanza mara moja ujenzi wa Soko Kuu la Kariakoo kwasababu tayari Serikali imepata fedha kiasi cha zaidi ya Sh. Bilioni 34 ambapo ujenzi huo utahusisha soko la zamani na kujenga mengine mawili mapya ya kisasa mkabala na soko la zamani la Kariakoo na kujenga soko jingine jipya katika eneo la Jangwani Jijini Dar es Salaam.