Na Jackline Martin,TimesmajiraOnline,Dar
UONGOZI wa miaka mitatu madarakani wa Rais Samia Suluhu Hassan, umeleta mageuzi makubwa kwenye kilimo, ikiamua kuwekeza kwa kiwango kikubwa fedh kwenye kuendesha shughuli za uzalishaji.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, mwishoni mwa wiki wakati wa futari iliyoandaliwa na Wizara kama sehemu ya maadhimisho ya miaka mitatu ya Rais Samia kuwepo madarakani.
Bashe alitumia fursa hiyo kueleza yale yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu.
Ameongeza kuwa bajeti ya kilimo imeongezeka kutoka sh. bil 290 kwa mara ya kwanza hadi sh. Bil 750 mwaka wa tatu, ambao adiyo huu tunaendelea nao ikafika hadi sh. bil 970 na tunataraji kwa mwaka ujao sekta ya kilimo bajeti inaweza kufika trilioni.
Aidha, amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani, eneo la umwagiliaji katika nchi yetu lilikuwa hekta 726,000. Alisema kwa mwaka wa kwanza Rais alitoa fedha bajeti ya umwagiliaji zisizozidi sh Bilioni 50 mpaka sh. Bilioni 361.
Amesema kwa mara ya kwanza tutaandika historia katika nchi yetu kwa kufanya mradi wa kwanza wa kutumia maji kutoka Ziwa Victoria baada ya kukamilisha upembuzi huu.
Kwa upande wa vijana, Bashe alisema Serikali yake haikutaka kuwalaumu vijana kwamba wamemaliza vyuo vikuu katafuteni kazi, kama tu sekta za umma na za binafsi haziwezi kuwaajiri.
“Changamoto ya kwanza ya vijana ikawa ni kupata ardhi, Rais Samia, mwaka jana wakati anazindua mradi wa BBT, niwaambie ukweli Watanzania, ardhi tuliyokuwa nayo kwa ajili ya kuwapa vijana ilikuwa ni hekari 300 tu, leo tuna jumla ya hekari 200,000 ambayo Serikali imeikusanya na imeinunua.” Amesema Bashe.
“Hatua ya kwanza Serikali imesajili vijana 800 wamepelekwa kwenye mafunzo baada ya kupitia machujio mbalimbali tumebaki na vijana 680, ambapo vijana 260 wamepelekwa shamba la Chinangali.
Katika shamba hili Serikali imejenga nyumba ambazo vijana wanaishi, inawapatia posho 150,000 kila mwezi na kuwalipia fedha ya chakula sh 200,000 kwa kila meja.”
Eneo la tatu la BBT ni ‘BBT Extension’.
Amesema Serikali imeingia makubaliano na Chuo Kikuu cha SUA. Vijana wanamaliza kutoka SUA, kisha sisi tunawaingiza kwenye makampuni yanayonunua Pamba, wanawaajiri na kuwalipa sh. 500,000 kila mwezi na mpaka sasa vijana 250 wameanza na tunaenda kwenye zao la tumbaku na mazao yote tutafanya hivyo na huu ni mradi unaofanywa na serikali pamoja na sekta binafsi.” alisema
“Leo anafanya upembuzi yakinifu wa mabonde yote tuliyonayo ya nchi hii. Inawezekana asiyakamilishe yeye, atakuja kuyakamilisha mtu. Na hiyo ndio vision ya muda mrefu,” amesema
Amesema Rais ameamua kuchukua mwelekeo sahihi kwenye kilimo. “Niwaambie Watanzania wote kwa zaidi ya miaka 60 tumekuwa tukifanya shughuli za kilimo kutatua matokeo,” Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.
Ujenzi wa mabwawa
Kwenye eneo hilo, Bashe alisema kwa mara ya kwanza mwaka huu Serikali ya Awamu ya Sita imeanza ujenzi wa mabwawa 100 kuvuna maji ya mvua yanayomwagika barabarani,” amesema Bashe.
Ameongeza kwamba lengo la Serikali ya Rais Samia ndani ya miaka saba ijayo ni kuchimba visima 67, 000 kwa ajili ya wakulima wadogo ambapo visima hivyo jumla vitatupatia ekari milioni 2.5 ambazo zitakuwa zinamwagiliwa lengo ikiwa ni kumfanya mkulima abaki shambani.”
“Eneo la nne kwenye BBT, ni visima, Rais mwaka jana alizindua mradi wa miaka saba wa kuchimba visima 67,000. Mradi wa visima malengo yake ni kuondoa adha kwa wakulima wadogo kutegemea kilimo cha mvua,” amesema Basshe na kuongeza.
“Mkulima atachimbiwa kisima, atawekewa tenki la lita 5,000 na vifaa vya umwagiliaji vya ekari 2.5. tumeshauza mradi huu Mbarali na baadhi ya maeneo ya Dodoma.”
Bashe ametaja eneo jingine ambalo Serikali iliamua kuweka fedha kwa wingi ni kuondoa upotevu wa mazao. Alisema Serikali ya Awamu ya Sita wakati inaingia madarakani upotevu wa mazao ya nafaka kwenye nchi yetu ilikuwa inafika asilimia 30. Kwa mujibu wa Bashe kiwango hicho kimepungua.
Pia, Bashe amesema eneo jingine ambalo Serikali ya awamu ya sita imeamua kuwekeza kwa nguvu ni ujenzi wa maabara za kupima afya ya udongo.
Amesema pamoja na hilo, Rais alitoa fedha ya kununua vifaa vya kupimia afya ya udongo kwa wakulima wa Halmashauri 142 bure nchi nzima.
“Na juzi mimi kama Waziri wa Kilimo kwa mara ya kwanza hata hapa kwenye simu yangu naweza kuangalia mkulima aliyepimiwa afya ya udongo katika wilaya yoyote katika nchi hii,” alisema Bashe.
Bei ya mazao
Kuhusu eneo hili, Bashe amesema, “Ukimuuliza mkulima changamoto kubwa anayokubaliana nayo, ni bei za mazao kuanguka.
Katika hatua hii, Serikali imeamua kuunganisha shughuli za mashambani na kuongeza mazao thamani. Mwaka jana tumepata shida ya bei korosho kwenye soko la Dunia na tumeauza korosho yetu kwa bei ya chini.
Njia pekee hapa ya kumsaidia mkulima na kuongeza thamani ya zao hili.
Kwenye hili serikali imeanzisha mradi unaitwa ‘MARANJE’ na mpaka sasa tunatumia wastani wa sh. Bil 10 kwa ajili ya kujenga MARANJE ambapo hapo, serikali inajenga maghala yatakayosubiri mwekezaji alete mashine tu kwa ajili ya kubangua korosho na malengo yetu ifikapo 2026/27 korosho yote ibanguliwe nchini.”
*Tanzania kuzalisha tani milioni 30
Kwenye eneo hilo, Bashe amesema lengo walilojiwekea kama Wizara ya Kilimo ni kuzalisha tani milioni 30 ya mazao ya chakula. “Na katika hali ya kawaida, hiyo ndio imeenda. Matokeo tunayoona kutoka mashambani, hali ni nzuri sana katika mashamba,” amesema Bashe.
More Stories
Mjumbe wa Baraza UWT ahimiza wananchi kuwachagua viongozi wa CCM
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa