Na Yusuph Mussa, Timesmajiraonline,Dodoma
MKURUGENZI Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Frank Nyabundege amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuiongezea fedha benki hiyo ili kukidhi mahitaji ya wakulima kwa kuendelea kukopa fedha ili kukuza kilimo na uchumi wao.
Kwani mwaka 2021 wakati anaingia madarakani, bajeti ya Wizara ya Kilimo ilikuwa sh. bilioni 294, lakini kwa sasa bajeti hiyo imefikia sh trilioni 1.2. Wakati kwa Benki ya TADB, mwaka 2021 walikuwa wana mtaji wa sh. bilioni 60, lakini sasa wana mtaji wa sh. bilioni 442.
Ameyasema hayo Agosti 5, 2025 wakati anazungumza na wakulima wa korosho na zabibu kwenye semina iliyotolewa na Wataalamu wa Benki ya CRDB kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nanenane yanayofanyika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
“Sasa hivi ninyi wakulima wa nchi hii ndiyo mnatakiwa kutembea kifua mbele kwa vile tunae kiongozi ambaye kwa utashi wake wa kisiasa amekuwa akihakikisha Sekta ya Kilimo inapewa kipaumbele kwa rasilimali fedha. Kwani mwaka 2021 wakati anaingia madarakani, bajeti ya Wizara ya Kilimo ilikuwa sh. bilioni 294, lakini kwa sasa bajeti hiyo imefikia sh trilioni 1.2. Wakati kwa Benki ya TADB, mwaka 2021 tulikuwa na mtaji wa sh. bilioni 60, lakini sasa tuna mtaji wa sh. bilioni 442, na hayo ni mafanikio yake ya miaka minne tu” alisema Nyabundege.

Nyabundege alisema wakati Rais Dkt. Samia anaingia madarakani mwaka 2021, wakulima wa korosho walikuwa wanazalisha tani 210,000 lakini kwa msimu huu mwaka 2025, wameweza kuzalisha tani 550,000, na hiyo imetokana na kuuziwa mbolea na viuatilifu kwa bei ya ruzuku, kwani imekuwa inatoa nafuu kwa mkulima, badala ya mfuko wa mbolea kununua kwa sh 140,000, mkulima anaununua kwa sh. 70,000.
“Ninyi wakulima mnatakiwa mtumie nafasi hii adimu, sio kila kiongozi anaengia madaraka atawajali wakulima. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani aliamua kuwekeza kwa wakulima na wafugaji, kwa kusema Watanzania wengi anaowangoza katika nchi hii ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Ili waweze kuneemeka alisema atahakikisha anawasaidia, na akaanza kuongeza bajeti kwenye Wizara ya Kilimo, bajeti kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi, na sisi Benki ya Maendeleo ya Kilimo akatuongezea mtaji.

“Na ninyi mnaopewa mafunzo haya ili muweze kuwezeshwa, kwani Rais ametuwezesha mtaji mkubwa sana. Na kati ya mtaji aliotuongezea ni mpaka wa kuzipatia benki nyingine, kwani sisi tunashirikiana na benki 19, hivyo wewe huko ulipo sio lazima utuone sisi, bali unaweza ukaenda benki ya jirani yako mfano NMB, CRDB, NBC, TCB ukawaelezea unataka mkopo unaodhaminiwa na Benki ya TADB, na ni kwa sababu Rais alitupatia fedha nyingi ili tuzipatie benki nyingine kwa ajili ya wakukima” alisema Nyabundege.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Afisa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya TADB, Angelina Nyansambo alisema, benki hiyo imeandaa mafunzo ya elimu ya fedha, uwekezaji, bima na maadili kwa wakulima wa korosho kutoka Itigi mkoani Singida na wakulima wa zabibu kutoka mkoani Dodoma. Lengo la mafunzo ni kuwajengea uwezo wqkulima wafanye kilimo cha kibiashara na kuwa na usimamizi mzuri wa mikopo.



More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako