January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aagiza wakuu wa mikoa, wilaya kushirikiana na TNBC

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira,Online, Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kushirikiana na Sekretarieti ya Baraza la Tiafa la Biashara (TNBC) kuhakikisha mikutano ya mabaraza ya Mikoa na Wilaya inafanyika, kwani ndio chimbuko la mapendekezo na mabadiliko kwa ngazi ya Taifa.

Ametoa agizo hilo jana wakati wa kufungua mkutano wa 12 wa TNBC uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Rais Samia amesema changamoto na mapendekezo mengi hutokea katika ngazi za Wilaya na Mikoa kwani ndiyo mahala biashara na uwekezaji unafanyika.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akifunga mkutano wa 12 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) lililofanyika katika ukumbi wa Kikwete Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 26 Juni, 2021.

“Nawataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha mikutano ya baraza ngazi ya Mkoa (RBC) na Wilaya(DBC) inafanyika mara kwa mara chini ya uenyekiti wao ili kuibua changamoto na mapendekezo yatakayoboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji hapa nchini,” amesema Rais Samia

Ameongezea kuwa yapo mambo yakuchukuliwa hatua kwa ngazi ya Wilaya au Mkoa yale yanayohusiana na sera, kanuni na sheria mbalimbali juu ya biashara na uwekezaji yanafikishwa katika ngazi ya taifa kujadili na kupatiwa majawabu.

“Kuna umuhimu mkubwa wa kuyafanya mabaraza ya mikoa na wilaya kuwa hai, kwani itasaidia kuibua fursa na kufanyiwa kazi,” amesema Rais Samia na kuongezea kuwa TNBC ihakikishe inafanya uratibu wa baraza haya.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa 12 wa TNBC, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema amepokea maagiza ya Rais Samia Suhulu Hassan na kusema atayatekeleza ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuhakikisha malengo ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo 2025 yanatekelezeka kwa vitendo.

Mawaziri pamoja na viongozi mbalimbali wa Taasisi pamoja na Wafanyabiashara wakiwa katika mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) lililofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam leo tarehe 26 Juni, 2021.

“Hivi karibuni tulizindua Baraza la Biashara la Mkoa wa Pwani na tuliweza kusikiliza kero, changamoto na mapendekezo mbalimbali kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji juu ya namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara kwa ngazi ya mkoa na hata taifaa,” amesema Kunenge

Ameeleza kuwa tayari ameshatoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya zote za mkoa wake kuhakikisha wanafanya mikutano ya mabaraza ya wilaya yatakayowezesha kuibua changamoto na mapendekezo yatakayofanyiwa kazi kwa ngazi ya wilaya, Mkoa, Wizara na Taifa.

“Huu ni muundo mzuri unaowakutanisha sekta binafsi na umma pamoja kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kuendelesha shughuli za biashara na uwekezaji kwa pamoja hali itakayosaidia kuinua mapato kwa Wilaya, Mkoa na Taifa kwa ujumla,” amesema Kunenge

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt.Godwill Wanga alisema mkutano wa 12 umefanyika kwa weledi mkubwa chini ya uwenyekiti wa Rias Samia Suluhu Hassan na kwamba maamuzi mengi yaliyotolewa yamelenga katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

“TNBC itaendelea kuratibu mikutano ya mabaraza ya Mikoa na Wilaya ikiwa ni pamoja na kutafuta rasilimali fedha zitakazo wezesha mikutano hii kufanya kwa weledi mkubwa chini ya uratibu wa Baraza lake,” alisema Dkt.Wanga

Kauli mbiu ya Mkutano wa 12 wa TNBC mwaka huu ulikuwa ni “Ufanisi wa Biashara na Uwekezaji katika uchumi wa kati”