December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia aagana na Balozi wa China

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo tarehe 4 Juni, 2021 ameagana na aliyekuwa Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke ambaye amemaliza kipindi chake.

Katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma, Rais Samia amemshukuru, Wang Ke kwa jitihada zake za kuendeleza na kukuza uhusiano wa Tanzania na China ambao umewezesha kutekelezwa kwa miradi mbalimbali iliyofadhiliwa na China hapa nchini ikiwemo maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, jengo la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki lililopo Jijini Dar es Salaam na msaada wa shilingi Bilioni 35 zilizoelekezwa katika miradi ya maendeleo.

Rais Samia pia amemshukuru kwa ufadhili wa China katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa huduma za kijamii pamoja na ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji ambao pamoja na kukuza pato la nchi umesaidia Watanzania wengi kupata ajira.

Mhe. Rais Samia amepokea salamu za Rais wa China Mhe. Rais Xi Jinping na amemtakia yeye na Wachina wote maadhimisho mema ya miaka 100 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) itakayotimia tarehe 01 Julai, 2021 na shukrani kwa uhusiano na ushirikiano mzuri kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na CPC, na uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na China uliodumu kwa miaka 56.

Ameeleza kuwa anatambua kazi kubwa iliyofanywa na CPC katika kuijenga China, kujenga na kuimarisha uhusiano wake na Mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania na amemhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano huo.

Kwa upande wake Mhe. Wang Ke amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa ushirikiano mkubwa alioupata kutoka Serikalini wakati wote wa kipindi chake cha Ubalozi na amempongeza kwa kupokea kijiti cha Urais kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.

Amewasilisha salamu za Rais wa China Mhe. Xi Jinping ambaye amesema ana imani kubwa kuwa Mhe. Rais Samia atafanya mazuri na makubwa kwa Tanzania kutokana na dhamira yake ya kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na Hayati Dkt. Magufuli hususani uendelezaji wa miradi ya kimkakati, kuchukua hatua madhubuti za kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuchukua hatua za kisayansi za kukabiliana na janga la ugonjwa wa Korona (Covid-19).

Amesema China itaunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais Samia na ameshukuru kwa salamu za heri na pongezi kwa chama cha CPC kutimiza miaka 100 ambapo pamoja na kufanya mageuzi na kuleta maendeleo makubwa kwa China kimekua kutoka wanachama 50 hadi wanachama Milioni 92 na kwa sasa kipo katika mchakato wa mageuzi mengine ya mfumo wake wa ujamaa wenye misingi ya Kichina utakaojenga nchi ya kisasa zaidi na kutoa elimu ya historia ya China kwa vijana wake.

Aidha, Mhe. Wang Ke amesema China ipo tayari kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na ugonjwa wa Korona.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Mbarouk Nassor Mbarouk.