January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Mwinyi azungumza na wadau wa mafuta, gesi

Na Penina Malundo,TimesMajira Online.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amefanya mazungumzo na wadau wa Sekta ya Mafuta na Gesi na kutoa maelekezo kuundwa kwa Chama cha Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi, Zanzibar.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo, Bodi ya Wakurugenzi wa Jumuiya ya Watoa Huduma wa Sekta ya Mafuta na Gesi (ATOGS) ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Abdulsamad Abdulrahim ilifanya kikao Zanzibar na kupata fursa ya kutembelea Ikulu na kufanya mazungumzo Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi ametoa maelekezo kwa Bodi ya ATOGS, kuhakikisha Zanzibar kupitia dira yake mpya ya Uchumi wa Bluu (2020/50 Blue Economy) inanufaika kiuchumi kupitia Sekta ya Mafuta na Gesi.

Pia amependekeza kuundwa kwa Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya
Mafuta na Gesi, Zanzibar na pia alielekeza sheria zilizoundwa hivi karibuni kusimamia rasilimali za mafuta na gesi kwa upande wa Tanzania Bara, ikiwemo Sheria ya Uwezeshaji Watanzania (Local Content Law), zitumike pia kwa upande wa Zanzibar badala ya kutengeneza sheria nyingine mpya.

“Naiomba ATOGS kuandaa warsha za pamoja zitakazolenga kutoa elimu ya viwango
vya kimataifa (capacity building) kwa taasisi mbalimbali za sekta ya umma na sekta binafsi Zanzibar, ikiwamo Shirika la Maendeleo ya Petroli Zanzibar (ZPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Mafuta Zanzibar (ZURA) na nyingine ili kuzijengea uwezo taasisi hizo kuhusiana na mambo mbalimbali kwenye Sekta ya Mafuta na Gesi, “amesema.

Nayo taarifa kutoka Bodi ya ATOGS iliyowasilishwa na Mwenyekiti Abdulsamad Abdulrahim imeeleza miongoni mwa mambo waliyozungumzwa kuwa ni kuona ni jinsi gani Zanzibar inaweza kunufaika na Sekta ya Mafuta na Gesi.

“Lengo kuu la ziara hiyo lilikuwa ni kumpongeza Rais Mwinyi kwa kuchaguliwa kwake kuwa rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi la Zanzibar katika
uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 27, 2020 pia ilikuwa ni ziara yenye lengo la la kuwatambulisha Wajumbe wa Bodi ya ATOGS na kuitambulisha rasmi ATOGS na shughuli zake hapa nchini,” amesema.

Aidha Abdulrahim amesema, Rais Dkt. Mwinyi kwamba ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wadau wa sekta binafsi Zanzibar ili kushauri kuundwa kwa Jumuiya ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi kwa upande wa Zanzibar ikiwa pamoja na kuandaa warsha za pamoja zitakazolenga kutoa elimu ya viwango vya kimataifa kuhusiana na Sekta ya Mafuta na Gesi kwa maslahi mapana ya wananchi wa Zanzibar na nchi kwa ujumla.

“Tuko tayari kuchukua au kupokea maelekezo kutoka kwa Rais wa Zanzibar na Serikali yake, jinsi gani
tunaweza kufanya kazi kwa pamoja na kuishauri Zanzibar kuhakikisha inanufaika na rasilimali za Mafuta na Gesi vilevile tumemueleza Rais kwamba kuna haja ya kuboresha sheria zinazosimamia rasilimali za Mafuta na Gesi nchini Zanzibar,” amesema.

Abdulrahim amesema japokuwa Zanzibar kuna sheria inayosimamia rasilimali hizo (Petroleum Act) lakini hawana sheria ya Uwezeshaji Watanzania na Kanuni zake (Local Content Law and
Regulations) hali ambayo inawakosesha wananchi fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana katika sekta ya uziduaji (Extractive Industry) nchini.

Abdulrahim amesema ATOGS inapongeza utayari wa Rais Mwinyi, katika kushirikiana na wadau wa Sekta ya Mafuta na Gesi nchini kwa ajili ya kuiwezesha Zanzibar kupiga hatua
kiuchumi kupitia Sekta ya Mafuta na Gesi.

“Tumemueleza Rais kwamba Jumuiya itakayoundwa ya Watoa Huduma katika Sekta ya Mafuta na Gesi ya
Zanzibar itafanya kazi kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi na wananchi,” amesema.